Katibu Mkuu Mkondo azindua Kamati ya Huduma ya Msaada wa Kisheria Pwani, atoa maagizo

NA ROTARY HAULE

KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Mkondo amezindua Kamati ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mkoa wa Pwani huku akiitaka kamati hiyo kufanya kazi kwa weledi,bidii na uaminifu.
Mkondo amezindua kamati hiyo Mjini Kibaha juzi mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mwanasha Tumbo na wadau mbalimbali wa msaada wa kisheria wakiwemo mawakili.

Mkondo amesema kuwa wizara imekuja na mkakati wa kuanzisha kamati za msaada wa kisheria katika mikoa mbalimbali ambapo mpaka sasa tayari mikoa sita imeunda kamati hizo.

Ametaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma,Arusha,Mwanza,Dar es Salaama katika Wilaya ya Temeke,Kinondoni na Pwani na kwamba mpango huo ni kuhakikisha unafika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Amesema,lengo la kuanzisha kamati hizo ni kuhakikisha huduma za kisheria zinapatikana kwa urahisi na haraka hususani katika kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo.

Mkondo amesema, maeneo makubwa ambayo kamati hiyo inapaswa kuyaangalia zaidi ni katika ukatili wa kijinsia,haki za watoto,migogoro mbalimbali ikiwemo ardhi,mirathi,yatima na wajane.

Amesema,wizara inatambua mchango mkubwa wa watoa huduma wa msaada wa kisheria hapa nchini ndio maana imefikia maamuzi ya kuunda kamati hizo ili kusudi kazi hizo zifanyike kwa wakati na haraka.
Aidha, Mkondo amesema kuwa kutokana na umuhimu huo wizara imelazimika kufuta viwango vya fedha za ada ya usajili kwa taasisi na wadau wa msaada wa kisheria ili kuweza kurahisisha utoaji wa huduma katika jamii.

"Wizara ya Katiba na Sheria inatambua umuhimu wa watoa huduma wa msaada wa Kisheria hapa nchini na ndio maana imeamua kufuta ada za usajili, lakini mategemeo makubwa ni kuona huduma hizi zinatolewa bure na kwa wakati,"amesema Mkondo.

Mkondo,ametoa wito kwa kamati hiyo kuhakikisha inaimarisha mawasiliano na ushirikiano baina ya watoa huduma,wadau na Serikali, kushirikisha jamii na kuzingatia haki hasa katika matendo ya unyanyasaji na vitendo vya ukatili.

"Yapo matukio mengi hususani ya watoto kunyanyaswa na kufanyika vitendo vya ukatili, kwa hiyo lazima wanasheria wawe mstari wa mbele kukomesha na kudhibiti vitendo hivyo,"amesema Mary Mkondo

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mwanasha Tumbo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuunda na kuzindua kamati hiyo kwani itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi katika kulinda haki zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Msaada wa Sheria Mkoa wa Pwani, Wakili Philemon Mganga,amesema kuwa watatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Mganga ameishukuru Serikali kwa hatua ya kuzindua kamati hiyo na kwamba atahakikisha anasimamia maadili na nidhamu kwa watoa huduma na yeyote atakayekwenda kinyume atachukuliwa hatua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news