KUMBUKIZI YA MWALIMU-2:Tanzania ni bima yatosha,Wasomi watukumbusha

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

MEI 5, 2022 kupitia Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambalo liliandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kufanyika katika ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam, wasomi waliweza kuyataja mambo mengi yanayomuhusu Mwalimu Nyerere yakiwemo ya kusisimua katika harakati mbalimbali za kuunganisha jamii kitaifa na Kimataifa.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga akitazama na kununua baadhi machapisho ya vitabu mbalimbali vya Mwalimu Nyerere baada ya kufungua Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 100 ya Kuzaliwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika mtazamo wa kiuchumi pamoja na uchambuzi wa vitabu lililofanyika kwenye ukumbi wa benki hiyo Mei 5,2022 jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mkuki na Nyota, Walter Bgoya ambapo alieleza alivyobahatika kufanya kazi katika miaka miwili ya mwisho wa maisha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Alisema, Mwalimu Nyerere alilipa kipaumbele suala la utu, usawa na haki katika kukuza amani na utulivu nchini, kwa sababu kusipozingatiwa kunaweza kuleta uvunjifu wa amani au vita katika Afrika.

Alisema, kutokana na kuendelezwa maono ya Mwalimu Nyerere, Tanzania imekuwa mahali salama na kimbilio la nchi rafiki za Afrika wakati wanapopata shida kwao kama nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nyinginezo.

"Na kuna wakati,Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema Tanzania ndio bima yao pale inapotokea shida katika mataifa yao,"amesema.

Naye Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kupitia kalamu yake anaendelea kukujuza mambo mengi mazuri yamhusuyo Hayati Baba wa Taifa kwa njia ya mashairi, ikiwa sehemu ya kwanza ya shairi hili ulijifunza jambo,SOMA HAPA

 Endelea shemu ya pili hapa chini, Tanzania ni Bima Tosha;

1:Wasomi watukumbusha, Nyerere wa Tanzania,
Alivyotuimarisha, na kujenga Tanzania,
Wengi alishirikisha, si kwamba twawasagia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

2:Amani tunadumisha, hapa kwetu Tanzania,
Inatutofautisha, nchi zatuzungukia,
Vurugu wavurumisha, hali twasikitikia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

2:Museveni hakubisha, aonavyo Tanzania,
Kwamba ni bima yatosha, choko zinapoingia,
Hapa wajisalimisha, amani ya Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

3:Sihitaji kukumbusha, kazi yetu Tanzania,
Vita kuwafurumusha, majirani Tanzania,
Kuyaokoa maisha, usalama Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

4:Kile alifurahisha, Nyerere wa Tanzania,
Litaka kutufikisha, kuwa huru Tanzania,
Kusiwe wa kututisha, uchumi wa Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

5:Kujitegemea bisha, kama siyo nzuri nia,
Ambayo ngesababisha, hakuna kuingilia,
Vile tunavyozalisha, ndivyo tungevitumia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

6:Kwa kweli alikiwasha, Azimio kuingia,
Mali alitaifisha, ziwe zetu Tanzania,
Japo hakutufikisha, yake tuliona nia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

7:Miiko alianzisha, viongozi Tanzania,
Wasije jimilikisha, mali za Watanzania,
Hizo pia lifundisha, kotekote Tanzania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

8:Wala rushwa liwarusha, mbali wende jifilia,
Alisema imetosha, kuongoza kaishia,
Somo alitufundisha, cheo si kung’ang’ania,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.

9:Wengi alitusomesha, shule kote Tanzania,
Bila ada kufupisha, kile ninakuambia,
Tungeshindwa jisomesha, tubaki twalialia,
Kumbukizi ya Mwalimu, hiyo ya vizazi vyote.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news