Mafuta ya ndege yapanda kutoka 1000/- hadi 3900/- kwa lita nchini Nigeria, mashirika ya ndege kusitisha safari Jumatatu 'NI MAUMIVU YA VITA VYA URUSI NA UKRAINE'

NA GODFREY NNKO

MASHIRIKA ya ndege nchini Nigeria yametangaza kuanzia Jumatatu ya Mei 9,2022 yatasitisha safari zote za ndani za anga kutokana na mafuta ya ndege kupanda mara nne zaidi ya awali.
Licha ya kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta barani Afrika, Nigeria huagiza kutoka nje karibia mafuta yote ya ndege.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Umoja wa Waendeshaji wa Mashirika ya Ndege ya Nigeria (AON).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyonukuliwa na Shirika la Habari la Reuters, uamuzi huo umefikiwa ili kujipa muda wa kutafakari zaidi kwa kuwa, bei zimepanda kutoka Naira 190 kwa lita hadi Naira 700.

Gharama inayotajwa ni mara nne ya bei ya awali, kwani inakadiriwa ni kutoka shilingi 1000 za Kitanzania hadi shilingi 3900 za Kitanzania kwa lita moja.

Safari za ndege za ndani nchini Nigeria zimetatizika tangu Machi, 2022 huku baadhi mashirika yakianza kughairi ratiba za ndani huku zingine zikichelewesha shughuli zao, kwa sababu ya uhaba wa mafuta ya ndege.

Bei ya mafuta Duniani imepanda kwa kasi kubwa siku za karibuni baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, hivyo kusababisha kuongezeka kwa soko la mafuta yasiyosafishwa, na kuathiri mashirika ya ndege, abiria na ongezeko kubwa la gharama.

Shirikisho hilo limesema katika taarifa hiyo kuwa, kutokana na gharama za mafuta,gharama ya nauli ya safari ya saa moja imeongezeka zaidi ya mara mbili hadi Naira 120,000, ambayo ni ngumu kuwapata wateja wa kulipia.

Abiria wanaotumia usafiri wa ndege nchini Nigeria hulipia nauli kwa kutumia Naira, ambayo imekosa nguvu kutokana na kushuka kwa thamani.

Wasambazaji wa mafuta hata hivyo wanalipwa kwa dola, fedha adimu katika uendeshaji wa shughuli nyingi za kiuchumi nchini humo na barani Afrika kwa ujumla.

Shirikisho hilo limesema kuendelea kupanda kwa gharama ya mafuta ya ndege kumezua mashinikizo ya uendeshaji ambazo zinatilia shaka uwezo wao wa kifedha.

"Kwa maana hiyo, Waendeshaji wa Mashirika ya Ndege ya Nigeria (AON) ... wanautaarifu umma kwa ujumla kwamba mashirika ya ndege wanachama yatasitisha kufanya kazi nchini kote kuanzia Jumatatu Mei 9, 2022 hadi taarifa nyingine itakapotolewa," ilisema sehemu ya taarifa iliyonukuliwa na Reuters.

Aidha,wasafiri wote wa ndani ya nchi wanaopanga kusafiri kwa ndege wameombwa kutafuta njia mbadala za safari zao kuanzia Jumatatu.

Post a Comment

0 Comments