Migogoro ya viongozi Tarime yamkwaza Waziri Bashungwa, aonya na kushauri

NA ANGELA MSIMBIRA,OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocennt Bashungwa amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kuacha migogoro isiyo na tija ambayo inachelewesha maendeleo kwa wananchi
Akiongea na viongozi hao jana wakati wa ziara yaka kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri hiyo, Waziri Bashungwa amesema, migogoro inayoendelea ya viongozi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inawanyima haki wananchi na kuchelewesha maendeleo kwa jamii.

Waziri Bashungwa amewataka viongozi hao kujenga mahusiano mazuri baina yao, lengo likiwa ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na wananchi wananufaika na miradi hiyo.
“Migogoro ya viongozi haijengi bali inabomoa umoja na ushirikiano uliopo, migogoro ikizidi wananchi ndio wanapata shida ya kukosa huduma bora , nawaagiza kuacha migogoro ambayo haina tija, wahudumieni wananchi,” amesisitiza Waziri Bashungwa.

Amesema, Serikali inaleta fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo ni wajibu wa madiwani kuhakikisha wanazisimamia Halmashauri kwa weledi ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kuleta matokeo chanya katika halmashauri.
Aidha, Waziri Bashungwa amewataka watumishi wa umma nchini kutimiza majukumu yao kwa weledi kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa Umma na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments