NMB yakutana na wadau wa utalii jijini Arusha

NA DIRAMAKINI

KATIBU Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Francis Michael amewataka wadau wa utalii mkoani Arusha kutumia fursa ya mikopo nafuu ya Benki ya NMB katika kuwekeza kwenye sekta ya utalii ili kuvutia wageni nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Francis Michael akisalimiana na wafanyakazi wa Benki ya NMB wakiongozwa na Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi (kulia) wakati wa kongamano la wadau wa utalii lililofanyika jijini Arusha. 

Akizungumza katika kongamano la utalii (Tourism Networking) lililofanyika jijini Arusha mwishoni mwa wiki Dk. Michael alisema Benki ya NMB imekuwa chachu katika kuhakikisha inawapa mikopo wadau wa sekta ya utalii katika kuimarisha mazingira ya vivutio nchini.

"Tunaomba mfanye jitihada za kuijenga sekta ya utalii kwani serikali imeshaweka mazingira ya kuitangaza kupitia filamu ya Royal Tour ambapo hadi sasa kuna baadhi ya hoteli zimeshajaa wageni, hivyo ni kitu cha kujivunia kwetu na nyie kama wadau ni vyema mkatumia fursa hiyo katika kuweka mazingira sawa," alisema Dk. Michael.

Dk. Michael aliwaeleza wadau wa utalii kutumia vema fursa waliyopewa na Benki ya NMB kwa sababu ni taasisi muhimu ya kifedha inayoshiriki kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi na ubunifu nchini.

Alisema, fedha watakazotengewa kwa ajili ya mikopo wazitumie vema ili wazirudishe na wengine wapate fursa ya kuzipata kwa ajili ya kukuza uchumi na kuongeza idadi ya watalii nchini kwa maendeleo ya sekta zote.

Alisisitiza kuwa, wadau wa utalii wahakikishe wanatumia vema fursa waliyopewa na NMB kikamilifu ili kuimarisha usalama kwa watalii wanapokua nchini, ikiwemo kutumia vituo vya polisi vinavyohudumia watalii lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii na kuwafanya wapate sababu za kurejea tena baada ya kurudi kwao.

“Hiki kinachofanywa na NMB ni kitu kikubwa sana, kifikirieni na mkitumie vizuri kwa sababu fursa kama hizi haziji mara mbili. Wafurahisheni watalii ili wakienda kwao wakawalete watu wengine na wao warejee tena na tena,” alisema Dk. Michael.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB - Filbert Mponzi akizungumza na wadau wa utalii wakati wa kongamano lililofanyika jijini Arusha. Benki ya NMB iliwakutanisha wadau wa utalii zaida ya 150 ilikujadili mbinu za kuboresha biashara zao. 

Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi alisema benki hiyo wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kuboresha sekta ya utalii nchini. Aidha, Mponzi alisisitiza kuwa kwa miaka ya hivi karibuni NMB imeanza kutoa huduma ya mikopo katika sekta ya utalii lengo ni kuimarisha katika kutoa huduma kwa wageni wanaofika nchini kutalii na kuona vivutio vilivyopo nchi nzima.

"Bado tunaendelea kutoa katika sekta ya utalii kwa lengo la kufanya vizuri zaidi na sasa tumejipanga kuwahudumia wageni wote wanaofika nchini, ili wakirudi kwao wapate sababu ya kurejea tena nchini," alisema Mponzi.

Benki ya NMB wiki kadhaa zilizopita walikutana na wadau wa utalii visiwani Zanzibar ambapo waliwaahidi kuwapa mikopo mbalimbali kuanzia maboti na miradi mingine itakayohamasisha watalii kutembelea visiwa hivyi vyenye utajiri wa historia na mambo ya kiasili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news