'Panya Road' wakalia kuti kavu Dar, msako waanza mtaa kwa mtaa

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla ameelekeza Jeshi la Polisi kuanza mara moja msako wa kuwakamata watuhumiwa wa wizi na unyang'anyi kwa kutumia silaha maarufu kama Panya Road na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo kufuatia taharuki iliyoibuka miongoni mwa wananchi baada ya kutokea kwa matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali ikiwemo Tabata, Chanika, Zingiziwa na Kunduchi ikihusisha vijana wa kati ya miaka 13 hadi 21.

Hali hiyo ndio imemlazimu RC Makalla kuhitisha kikao kazi cha kukabiliana na uhalifu huo kikihusisha na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Wilaya, Wakuu wa Usalama, Makamanda wa Wilaya zote za Kipolisi, Wakuu wa Vituo vya Polisi na Maafisa Polisi Jamii wa Kata na kuwapatia maelekezo.

Miongoni mwa maelekezo aliyotoa RC Makalla ni pamoja na kamati za ulinzi na usalama ngazi ya wilaya kufanya kikao na wenyeviti wote wa mitaa usika ajenda ikiwa kudhibiti uhalifu.

Aidha, RC Makalla ameelekeza OCD, wakuu wa vituo vya Polisi na Polisi Jamii kuongeza doria za mitaa kwa kutumia magari na pikipiki ambapo pia ameelekeza kila mkoa wa kipolisi kutoa taarifa ya mwenendo wa operesheni kila siku.

Hata hivyo, RC Makalla ameelekeza Jeshi la Polisi kuanza msako wa kuwakamata wanunuzi wa mali za wizi huku akiwataka wakuu wa wilaya kuweka utaratibu mzuri wa kuanza kuwatumia askari mgambo katika kuongezea Nguvu Jeshi la Polisi.

Pamoja na hayo RC Makalla ametoa wito kwa Wananchi kuondoa hofu kwakuwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi limejipanga kudhibiti uhalifu wowote.
RC Makalla akiwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa,Lawrence Malangwa upande wa kushoto na Kamanda Jumanne Muliro kulia wakati wa Kikao Kazi Anatoglo Mnazimmoja jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam , Jumanne Muliro amesema jeshi hilo limejipanga kutekeleza maelekezo ya RC Makalla ambapo amesema tayari wanawashikilia watuhumiwa mbalimbali

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news