Rais Dkt.Mwinyi:SMZ inathamini mchango wa Jumuiya ya Magoa Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa Jumuiya ya Magoa Zanzibar katika kuendeleza shughuli za maendeleo zikiwemo huduma za kijamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Magoa Zanzibar walipofika Ikulu jijini Zanzibar leo Mei 21, 2022, ujumbe ambao ulifika kwa lengo la kijitambulisha, mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Jumuiya ya Magoa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Bi. Amanda Demello.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, Jumuiya ya Magoa Zanzibar kama zilivyo jumuiya nyingine imekuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono Serikali kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za biashara, huduma za kijamii, uwekezaji na hata sekta ya utalii.

Hivyo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo katika kuhakikisha inatekeleza vyema shughuli zake zikiwemo huduma zake za kiroho kwa azma ile ile ya kuendeleza amani na utulivu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kwamba, ni jukumu la Serikali katika kuwapelekea wananchi huduma muhimu za kijamii lakini kutokana na uwezo wake kuwa mdogo jumuiya kama hizo zimekuwa zikiiunga mkono Serikali kutoa huduma hizo kwa wananchi jambo ambalo ni la msingi na la kupongezwa.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba, ujio wa jumuiya hiyo Ikulu na kupata fursa ya kuzungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kueleza changamoto walizonazo ili kuimaria uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Serikali na jumuiya hiyo.

Akizungumzia juu ya suala la uwepo wa mapapasi ambao wamekuwa wakiwasumbua wageni wanaotembelea Mji Mkongwe pamoja na fukwe mbalimbali katika visiwa vya Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa kupitia kikosi maalum cha askari wa utalii katika kuhakikisha mambo kama hayo hayatokei kwani yanaitia dosari sekta hiyo hapa nchini.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alitilia mkazo suala la kupewa kipaumbele kwa somo la historia katika skuli za Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba sekta ya utalii ambayo ndio sekta muhimu katika uchumi wa Zanzibar inahitaji historia hasa kwa utalii wa Zanzibar ukiwemo Mji Mkongwe.

Hivyo, Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kueleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuupitia upya mfumo mzima wa elimu ya Zanzibar ili iweze kuleta mabadiliko makubwa na kurudi katika hadhi yake kama ilivyokuwa hapo kabla.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Magoa Zanzibar, Bi.Amanda Demello alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuipa Jumuiya hiyo fursa ya kukutana nae na kuweza kubadilishana nae mawazo.

Akieleza historia fupi, Bi.Amanda alieleza kwamba Magoa walianza kuingia Zanzibar mnamo karne ya 18 kutoka Goa, nchini India kwa kutumia majahazi na meli za abiria.

Aliongeza kuwa katika karne ya 20 Magoa waliongezeka na kuwa wengi zaidi katika visiwa vya Zanzibar, Unguja na Pemba na kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya Mapinduzi na baada ya Mapinduzi

Katika maelezo yake, Bi.Amanda alitumia fursa hiyo kueleza changamoto inazoikabili jumuiya yao ikiwa ni pamoja na kukosa sehemu ya kukutana pamoja na kufanya shughuli zao kama ilivyo kwa jumuiya kama hiyo kwa upande wa Dar es Salaam, Arusha, Nairobi, Tanga na Mombasa.

Hivyo, Mwenyekiti huyo alieleza kwamba Jumuiya ya Magoa walioko Zanzibar ina matumaini makubwa na Serikali anayoiongoza Rais Dkt.Mwinyi kwani wanakubaliana na maendeleo yaliyofanyika kwa muda mfupi aliokaa madarakani na wanazikubali juhudi anazozichukua za kimaendeleo na kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa kitu kimoja.

Nae Bwana Wolfango Bosco Martins (Bulu), alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Magoa hapa Zanzibar pamoja na shughuli mbali mbali wanazozifanya na zile ambazo waliwai kuzifanya wao na wazee wao zikiwemo za utumishi Serikalini.

Post a Comment

0 Comments