Rais Samia afunguka ya moyoni, asisitiza umuhimu wa ziara za nje

NA GODFREY NNKO

“Wanataka tujifungie hapa, halafu walie ukata mifuko ipo mitupu, sina miujiza ya kujaza mifuko yao, lazima tutoke tukatafute;
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia mahojiano maalumu na Tido Mhando wa runinga ya Azam yaliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma huku akisisitiza kuwa, anatoka kwa kuwa safari zina faida nyingi kwa nchi ikiwemo kufungua biashara.

Mheshimiwa Rais Samia amewataka wanaokosoa safari zake nje ya nchi, wafanye tathmini ya safari hizo kabla ya kukosoa kwa kuwa zimekuwa na manufaa mengi kwa Tanzania.

"Wafanye tathmini za safari zenyewe, kila ninapoenda ninakuwa na wafanyabiashara, mfano nilikuta vikwazo 64 Kenya na vyote tulitatua baada ya kuzungumza,”amesema Mheshimiwa Rais Samia huku akigusia kuwa safari zake za Marekani alisaini mikataba ambayo kama itatekelezwa Tanzania itaingiza shilingi trilioni 11.

Mheshimiwa Rais Samia amefafanua kuwa,alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, safari yake ya kwanza aliifanya nchini Kenya, ambako kwa kushirikiana na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, walifanikiwa kuondoa vikwazo 64 vya kibiashara vilivyokuwepo kati ya Tanzania na Kenya.

Tujikumbushe Kenya

Ziara ya Mheshimiwa Rais Samia ya siku mbili ambayo ilifanyika mwezi Machi,2021 nchini Kenya ilifungua fursa mbalimbali na kuimarisha zaidi uhusianao baina ya pande hizo mbili.

Mheshimiwa Rais Samia wakati akilihutubia Bunge la Kenya mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya alisema; "Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni wapinzani, mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake, hawa ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu.

"Ni bahati mbaya kuwa watu hawa wapo katika pande zote mbili, Kenya na Tanzania hutokea pia wachache wao wakawa ni watumishi wa Serikali zetu na hata wanasiasa wa pande mbili za nchi zetu. Bahati nzuri ni kuwa si wengi ndio maana uhusiano wa nchi zetu mbili unatimiza miaka 56 sasa," alisema Samia.

Mheshimiwa Rais Samia aliahidi kwamba katika uongozi wake atahakikisha kuwa Kenya inabaki kuwa ndugu, jirani, mshirika wa mkakati ambao utafanya uhusiano kati ya nchi hizo mbili umefungwa katika mambo matatu.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni undugu wa damu ambao hauwezi kutenganishwa na mipaka ya kuchorwa kwenye ramani, suala la kihistoria na kijiografia.

"Ushirikiano wetu si wa hiari bali wa lazima kutokana na kanuni ya uasili wa undugu ambao Mwenyezi Mungu ameuumba, ushirika na ujirani yote yanatufanya tuwe pamoja na hatuna uwezo wa kulibadilisha kilichobaki ni tupendane au tuchukiane hatuwezi kukwepa kutokana na mambo haya matatu yaliyowekwa pamoja, tunategemeana kwa kila hali iwe kheri au shari,"alisema.

Rais Samia alisema, lengo lake ni kuhakikisha kwamba wawekezaji wa kigeni wanajenga imani ya kuwekeza nchini Tanzania na ili kurahisisha hilo serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ya miundo mbinu kama barabara, reli na bandari ili kupunguza gharama ya kufanya biashara .

Katika Bunge, Mheshimiwa Rais Samia alifafanua kuwa ziara hiyo ya kiserikali ya siku mbili nchini Kenya ilikuwa yake ya kwanza tangu aapishwe kuwa Rais, akisema ziara ya awali nchini Uganda haikuwa ziara ya kiserikali bali ni ilikuwa ya kusaini mikataba ya kibiashara.

Endelea na mahojiano

Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa,awali kulikuwa na sintofahamu ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo malori kuzuiwa mipakani kwa muda mrefu, kuchomwa kwa vifaranga vya kuku na mahindi kuzuiwa kutokana na madai ya kuwa na sumukuvu.

“Lakini nilipokwenda tukazungumza, tukaondosha vikwazo vile vyote, sasa hivi biashara kati ya Tanzania na Kenya imekua maradufu, na imekuwa zaidi kwa upande wetu,”amesema Rais Samia.

Baada ya kutoka Kenya alisema alikwenda nchini Uganda, ambako nako kulikuwa na shida kidogo kwenye mradi wa bomba la mafuta na tatizo hilo liliondolewa na mradi unaendelea na kisha akaenda Umoja wa Ulaya, ambako nako kulikuwa na miradi ya Tanzania iliyokwama, lakini sasa inaenda vizuri.

Amesema safari zake anakwenda na wafanyabiashara na kuwakutanisha na wafanyabiashara wenzao, ambako kumesainiwa mikataba kadhaa ya ushirikiano.

“Juzi tumerudi kutoka Marekani, tumesaini mikataba ambayo kama itatekelezwa kila mkataba karibu Sh trilioni 11. Wafanye tathmini enzi hizo hatuendi biasahara ilikuwaje ndani na sasa tunakwenda biashara ikoje,”amesema Rais Samia.

Akizungumzia Urais

Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, “Sidhani kama kuna mtu anaweza kusema ni fundi katika nafasi ya Urais, labda kama mimi ni mgeni kwa kuwa nina mwaka mmoja.

“Nilipoteuliwa kuwa Rais mshtuko ulikuwa tukio la msiba haikuwa Urais kwa kuwa nilikuwa Makamu Rais kuna mambo nilikuwa nayajua,”amesema Mheshimiwa Rais Samia katika mahojiano na runinga ya Azam.

Kuhusu Miradi

Mheshimiwa Rais Samia akizungumzia miradi mikubwa ambayo ilikuwa ikitekelezwa wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli amesema ilikuwa yenye tija ingawa changamoto ilikuwa ikiendeshwa kwa fedha za mikopo.

“Miradi ilikuwa ya kwetu kwa kuwa nilikuwepo katika Awamu ya Tano na nilikuwemo katika mipango na utekelezaji, changamoto ni ukubwa wa miradi na uwezo wetu wa ndani. Kwa tafsiri ni kuwa tumeijenga kwa fedha zetu lakini tulikopeshwa, tatizo ni itaendeleaje? Lakini ni miradi yenye tija,”amesema.

Royal Tour

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, kupitia vipande vya kuitangaza filamu ya Royal Tour ambavyo vimekuwa vikirushwa kwa miezi mitatu sasa vimeleta faida kubwa ambayo ni zaidi ya kiasi kilichotumika kuandaa filamu hiyo.

“Ni fedha nyingi, lakini faida zake zikianza kuingia wataona, kuhusu waliochangia juzi Arusha niliwashukuru kwa ujumla, lakini nitawataja tu,”amesema Mheshimiwa Rais

Mafuta ya Kula

“Mwaka 2020 mabadiliko ya tabia nchi hatukufanya kilimo vizuri, bajeti ya 2019/20 tulipandisha kodi ya mafuta yanayoitwa crude ambayo hayakuwa na kodi. Mafuta yakawa hayaingizwi, nazi na chikichi hazikutosheleza soko, hivyo bajeti inayokuja tunaenda kupitia mfumo wote wa kodi, tutaondoa kodi ya mafuta ya kula ili walete crude oil tuichakate tupate mafuta tuyasambaze ndani,”amesema Rais Samia.
Mafuta mengine

“Kwa Kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki, Tanzania tupo pazuri, hata kwa Afrika Mashariki sisi hali ya maisha ni nzuri ukilinganisha na majirani zetu.Kwetu bei za mafuta ni nzuri zaidi kuliko mafuta yanavyouzwa Marekani, lakini watu hawataki kutafuta ukweli, wanapiga kelele za kienyeji. Tanzania hatuagizi chakula, kipo cha kutosha,”amesea Mheshimiwa Rais Samia.

Tujikumbushe Kilichojiri Marekani

Hivi karibuni Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba saba kati ya makampuni ya Marekani na Tanzania yenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji mkubwa nchini.

Mikataba hiyo na makampuni makubwa ya Marekani iliyotiwa saini jijini Washington D.C. ina thamani ya Shilingi Trilioni 11.7 inayotarajiwa kutengeneza jumla ya ajira 301,110 kwenye kilimo, utalii, biashara na sekta nyingine za uchumi.

Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano (MoU), barua za kuonesha nia (letters of intent) na kuanza kwa mazungumzo ya uwekezaji na biashara kati ya makampuni ya nchi hizo mbili.

Miradi mingine iliyotiwa saini inalenga kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani katika kanda ya kaskazini ya sekta ya utalii wa Tanzania, ikiwemo kwenye maeneo ya kutangaza utalii na kuongeza idadi na ubora wa huduma zinazotolewa.

Rais Samia pia alishuhudia makampuni ya Marekani yakitangaza nia na mipango ya kuongeza mahusiano yao na Tanzania kwenye maeneo ya uwekezaji na biashara. Makampuni hayo ni pamoja na Upepo Energy, Astra Energy, Crane Currency na Parallel Wireless.

Pamoja na mikutano mingine, Rais Samia alihudhuria mkutano kwenye makao makuu ya Chemba ya Biashara ya Marekani (U.S. Chamber of Commerce) uliohudhuriwa na wafanyabiashara na viongozi wa serikali wa nchi zote mbili wakijadiliana namna ya kuongeza uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Marekani.

Ziara ya Ulaya

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia hivi karibuni amesema kuwa, ziara yake katika nchi za Ubelgiji na Ufaransa imekuwa ya mafanikio makubwa kwa Tanzania kutokana.

Alizitaja faida hizo kuwa ni ni kukwamua miradi iliyokwama, ukarabati wa Terminal II, Mabasi ya umeme kuanzishwa Dodoma na Dar es Salaam, uwezeshaji wa Afrika kutokana na athari za Uviko-19, fursa za mafunzo kwa Watanzania barani Ulaya na fedha za kukamilisha mradi wa mwendokasi na shughuli za kilimo.

Aliyabainisha hayo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, akitokea Ufaransa na Ubelgiji alikokwenda kwa ziara ya kikazi.

Alisema ziara yake nchini Ufaransa aliifanya kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron ili kushiriki mkutano wa ‘One Ocean’ wenye dhamira ya namna ya kuzitumia bahari duniani kiuchumi na ulinzi.

Mheshimiwa Rais Samia alibainisha kwamba, katika mkutano huo walijadiliana kwa pamoja na kwamba bado mijadala mingine inaendelea ili kufikia mwafaka wa namna ambavyo ulimwengu unapaswa kufanya juu ya rasilimali bahari.

Alieleza pamoja na mkutano huo, akiwa nchini humo alifanya ziara ya kiserikali ambapo alikutana na Rais Macron na wafanyabiashara wa nchi hiyo.

Mambo mazuri

“Tukiwa Ufaransa kama alivyosema Mkuu wa Mkoa (Amos Makalla) kuna vijipesapesa tumevipata pale kwa ajili ya kumalizia njia zetu za mwendokasi na tumepata pesa kwa ajili ya shughuli za kilimo,”alisema.

Mheshimiwa Rais alieleza wakati wakijadiliana kuhusu mradi wa mwendokasi aliulizwa kwamba haiwezekani Dar es Salaam au Dodoma kukawa na mabasi ya kwenda kwa umeme.

“Nikawaambia inawezekana sana kwa hiyo hilo lipo katika mazungumzo na baadaye tutakuwa kama Ulaya miaka minne mitano, sita ijayo tutafika huko,”alisema Mheshimiwa Rais Samia.

Ukarabati Terminal II

Alisema akiwa nchini Ufaransa alitia saini mkataba wa ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Terminal II ambayo awali ilijengwa na Wafaransa, hivyo wamekubaliana watakuja kuifanyia ukarabati.

“Walivyosema itaishinda Terminal III, kwa hiyo mkataba tayari kampuni tumeshasainiana nayo karibuni watakuja na wataanza,” alisema.

Mafunzo

Alieleza akiwa nchini Ubelgiji alifanya mazungumzo na serikali na Umoja wa Ulaya (EU), ambapo katika serikali wamekubaliana kuwekeana mkataba katika suala la mafunzo.

“Nafasi za mafunzo zilikuwa zinatangazwa tu, watu wetu wanaomba 20 kwa Tanzania, lakini sasa tumewaambia ili tufuatilie vizuri tuwekeane mkataba nap engine idadi ya hizo nafasi izidi tunaendelea na mazungumzo mkataba tutasaidi baadaye,” alisema.

Wafanyabiashara

Alisema katika nchi zote walifanya mazungumzo na wafanyabiashara na kutia saini mikataba kadhaa, kwamba chemba ya Tanzania na za biashara za mataifa hayo zilisaini ushirikiano.

“Hivi karibuni tunatarajia kupokea ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ufaransa na Ubelgiji waone wapi wanaweza kuja kuwekeza, imani yangu ni kwamba pale ambapo sekta binafsi inaweza kuwekeza serikali hatuwezi kuweka fedha yetu tutaitumia kwa mengine ambayo sekta binafsi haiwezi kuwekeza,” alisema.

Alisema bila kufanya hivyo Tanzania itachelewa kupata maendeleo na kufafanua kwamba msingi wa kuendelea haraka ni kushirikiana na wengine kama dunia inavyokwenda.

Kukwamua miradi iliyokwama

Kwa mujibu wa Rais Samia, kulikuwa na changamoto ya uhusiano na EU uliosababisha kukwama kwa baadhi ya miradi, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Shinyanga na Pemba na Miji ya Kijani ambayo ni Pemba na Kigoma.

“Kama mnavyojua katikati hapa tulichokozana kidogo na EU tulitetereka pesa za miradi zilikwama, lakini tumeshakwamua fedha za mradi mmoja umeshasainiwa na mwingine hivi karibuni kazi zitaendelea,” alisema.

Alisema katika mkutano wa Jumuiya ya Afrika (AU) na EU alioshiriki fedha Euro bilioni 150 zimetengwa kwa ajili ya Afrika.

“Hizo sasa ni kinyang’anyiro kwa Afrika atakayewahi mwanzo kupeleka miradi ya maana ndiye atakayepata fungu kubwa, kwa hiyo nasi tunajitayarisha tumeanza kupeleka michache tukiwa pale lakini tutajiweka vizuri tupeleke ili nasi tumege hilo fungu,” alisema.

Alibainisha kwamba katika mkutano huo walizungumzia masuala ya amani, usalama wa wahamiaji na ushirikiano wa kimataifa.

Uwezeshaji

Kuhusu uwezeshaji wa Afrika kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Uviko-19), alisema nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimetengewa Euro bilioni 55 ili kila taifa kwa wakati wake liende kuzungumza.

“Mazungumzo yangu nimevuna kama Euro 450 kwa miradi ambayo tutakwenda nayo kwa miaka mitatu,” alisema.

Alieleza katika ziara hiyo pia alikutana na baadhi ya watanzania wanaoishi nje ya nchi na kubainisha kwamba atayafanyia kazi maombi yote waliyoyawasilisha kwake.

“Kama mnavyojua sasa hivi tunafanya mapitio ya sera ya mambo ya nje na kipengele kikubwa ni kuwatambua ndugu zetu Watanzania walioko nje na kuwapa hadhi maalumu,”alibainisha Mheshimiwa Rais Samia.

Alisema sera hiyo ipo katika hatua za mwisho za marekebisho ili iwasilishwe serikalini, kisha bungeni kupitishwa na watanzania wanaoishi nje ya nchi kuanza kunufaika nayo ikiwemo kutambulika nchini.

“Kwa ufupi hayo ndiyo tuliyoyafanya pamoja na mengi mengine, lakini makubwa ndiyo hayo niwashukuru sana kwa mapokezi haya naomba mniruhusu sasa nikapumzike,”alisema Mheshimiwa Rais Samia.

Post a Comment

0 Comments