RC Kunenge:Chanjo ya Polio ni muhimu, wazazi hakikisheni watoto wanaipata

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka wazazi waliopo mkoani humo kuhakikisha wanakimbilia fursa ya kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ya ugonjwa wa kupooza (Polio) ili kukabiliana na mlipuko.
Kunenge ametoa wito huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kampeni maalum ya kutoa chanjo hiyo inayotarajiwa kuanza leo Mei 18, mpaka Mei 21,mwaka huu.

Amesema kuwa,kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa Polio inayoanza leo Mkoa wa Pwani itahusisha watoto wote walio na umri chini ya miaka mitano na kwamba wazazi lazima wahakikishe watoto wao wanapata chanjo hiyo.

"Kampeni hii ya utoaji chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Polio itaanza kutolewa leo Mei 18 na itaendeshwa nyumba kwa nyumba kwa watoto chini ya miaka mitano,nawaomba wazazi wajitokeze kushiriki kampeni hii ili kulinda afya za watoto dhidi ya ugonjwa huu,''amesema Kunenge.

Kunenge amesema, ugonjwa wa Polio ni mbaya na madhara yake ni makubwa kwani husababisha ulemavu wa ghafla wa viungo huku ukiathiri zaidi watoto chini ya miaka mitano.
Amesema,mtoto akipata chanjo ya Polio anakuwa salama kwakuwa tayari anakinga ya ugonjwa huo hivyo ni vyema kila mzazi akatambua umuhimu wa kuhakikisha mtoto wake anapata chanjo hiyo.

"Ugonjwa huu huathiri zaidi watoto chini ya miaka 15 ,hivyo ufuatiliaji wa watoto wa umri huo wanaopata ulemavu wa ghafla utaimarishwa ili wapatiwe matibabu stahiki,"amesema Kunenge.

Aidha Kunenge, amesema ili kupata Kinga kamili ya ugonjwa huo, chanjo itatolewa kwa dozi nne ambapo dozi ya kwanza hutolewa mtoto anapozaliwa na ya pili inatolewa katika umri wa wiki Sita,wiki 10 na wiki 14.

Amesema kuwa, kwa Mkoa wa Pwani chanjo hiyo itatolewa kwa jumla ya watoto 200,967 ambapo watoto wote chini ya miaka mitano wapata bila kujali kama walishapata chanjo hiyo .
"Wazazi wenye watoto ambao hawajapata kabisa chanjo na ambao hawakukamilisha ratiba ya chanjo nawasisitiza kuwepo majumbani tarehe hizo na endapo tarehe hizo zitapita pasipo kufikiwa na huduma hii basi waende katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo karibu yao,"amesema Kunenge.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Gunini Kamba,amewaomba wazazi hao kutoa ushirikiano kwa waratibu watakaopita katika nyumba zao kwa ajili ya kutoa chanjo hiyo kwakuwa jambo hilo linalenga kunusuru maisha ya familia zao.

Hata hivyo ,Kamba amesema chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote huku akiwataka wazazi kuacha kupotoshwa na maneno ya watu wachache wenye dhana potofu juu ya chanjo hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news