RC Kunenge:Daraja la Mto Wami pia liwe kivutio cha utalii na ni tunu ya Taifa

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge ametaka Daraja la Mto Wami kufanywa sehemu ya kivutio cha Utalii na ni Tunu ya Taifa.
Ameyasema hayo alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo lililopo Wami-Chalinze wilayani Bagamoyo ambalo ujenzi wake utarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka huu.

Kunenge amesema kuwa, daraja hilo la kimkakati ambalo limeghatimu kiasi cha shilingi bilioni 75.1 ambapo ujenzi umefikia asilimia 91 litakuwa kivutio kikubwa.

Amesema kuwa, pia daraja hilo ni muhimu sana kiuchumi ambapo lile la zamani lina changamoto nyingi za magari kupata ajali kutokana na namna lilivyojengwa.

Aidha, amesema kuwa daraja hilo linaunganisha mikoa ya Kaskazini na nchi jirani ya Kenya, hivyo ni kiungo muhimu wa kiuchumi kwani la zamani lilikuwa jembamba na magari hayawezi kupishana hubidi kusubiriana.

Amebainisha kuwa, anaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha na kusimamia miradi mikubwa na kuahidi kuikamilisha kwa wakati.

Aliongeza kuwa Daraja hilo kwa hapa nchini ndiyo litakuwa refu na baada ya kukamilisha daraja hili ambalo barabara zake ujenzi wake uko asilimia 80 watarekebisha lile la zamani kwa kipindi cha miezi mitatu na kukabidhi kazi zote Novemba mwaka huu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Ally alisema kuwa daraja hilo litakuwa mkombozi kwa wanabagamoyo kiuchumi na hakutakuwa na vifo vilivyokuwa vikitokea kwenye daraja la zamani.

Kwa upande wake mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANRODS), Evelyn Mlai amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 510 na nguzo zenye urefu wa mita 52 ni tofauti na lile la zamani lenye urefu wa mita 80.

Mlai amesema kuwa, barabara zake za miinuko zilizoboreshwa zina urefu wa kilomita 3.8 kutoka upande wa Chalinze na upande wa kutokea Tanga na daraja hilo linajengwa kwa teknolojia mpya ni madaraja machache hapa nchini pia mradi huo umetoa ajira kwa watu 390 ambapo asilimia 94 ni wazawa huku asilimia nne ikiwa ni wageni na linajengwa na kampuni ya China Power likisimamiwa na Ilshin ya Korea ikishirikiana na kampuni ya wazawa ya Advance Solution Engineering.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news