RC Kunenge:Ni marufuku kusafisha mashamba kwa moto

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amepiga marufuku wakazi wa mkoa huo kuacha kupalilia au kusafisha mashamba kwa kuchoma moto ili kuepusha uharibifu wa mali na mazingira.
Kunenge ameyasema hayo wilayani Mkuranga wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Zimamoto kwa mkoa huo, kwani uchomaji huo umeleta athari kubwa zikiwemo za kimazingira.

Amesema kuwa, uchomaji moto imekuwa ni changamoto kubwa aimbapo utaratibu wa uchomaji umekithiri.

"Usafishaji au upaliliaji wa kutumia moto unaharibu mazingira na kuleta umaskini, kwani baadhi wamejikuta wanaleta athari kubwa na uharibifu wa mali na misitu hivyo waache tabia hiyo,"amesema Kunenge.

Aidha, amesema kuwa ili kudhibiti hali hiyo ametaka wananchi kuendelea kupatiwa elimu ya kuachana na uchomaji holela wa moto na kukabiliana na kujikinga na changamoto na majanga ya moto.

Naye Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Jenifa Shirima alisema kuwa wamedhamiria katika kipindi hicho cha Wiki ya Zimamoto kuifikia jamii ya Mkoa wa Pwani kwa asilimia 70 kwa kuwapatia elimu ya tahadhari ya kujikinga na moto kwa makundi makubwa na madogo kwa kuyapatia elimu hiyo.

Shirima amesema kuwa, maadhimisho mwaka huu kauli mbiu yake inasema uchumi imara utajengwa kwa kuzingatia kinga na tahadhari dhidi ya moto ambapo lengo ni kuifikia jamii kuipatia elimu sahihi ya kujikinga na majanga pamoja na umuhimu wa kuwa na vifaa vya kugundua na kungamua ili kupambana na majanga ya moto.

Amesema kuwa majanga ya moto yamegharimu mali na maisha ya watu wengi na wakati mwingine kuleta athari za kiuchumi kwa taifa kutokana na hali hiyo wakaona kuna umuhimu sana wananchi kupata elimu ili kupunguza au kumaliza kabisa majanga ya moto.

Post a Comment

0 Comments