Serengeti Girls yasonga mbele kuwania tiketi ya Kombe la Dunia

NA DIRAMAKINI

TIMU ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls imefanikiwa kusonga mbele Raundi ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Kombe la Dunia baadaye mwaka huu India licha ya kuchapwa 2-1 na Burundi jana Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.
Ni mtaji wa ushindi wa 4-0 kwenye mchezo wa kwanza katikati ya mwezi uliopita unawafanya Girls wasonge mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-2 na sasa watamenyana na Cameroon katika Raundi ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya India katika Fainali ambazo zitaanza Oktoba 11 hadi 30.

Awali Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe, Mohamed Mchengerwa aliwatakia kila la heri wachezaji wa Taifa ya wanawake U 17 ya Serengeti Girls kufanya vizuri kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Burundi.

Mhe. Mchengerwa alizungumza na wachezaji wa Serengeti muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ambapo amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana matarajio makubwa na timu hiyo.

Alisema kuwa, anatambua kuwa timu hiyo ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Burundi mjini Kigali lakini isibweteke na badala yake itoke na ushindi wa kishindo ili kuwaogopesha Cameroon.

Ameahidi kuwa baada ya mechi hii atakwenda kuwaona na kuwashukuru kwa niaba ya Mhe. Rais na kuandaa chakula cha pamoja.

"Ni matarajio yetu kuwa timu ya Serengeti ikifuzu tutakuwa tumeziingiza timu mbili kwenye mashindano ya kombe la Dunia baada ya timu ya soka ya walemavu ya Tembo Warriors,"amesema.

Amesisitiza kuwa baada ya ushindi wa leo Serikali itaendelea kutoa kila msaada unaotakiwa ili timu izidi kufanya vizuri zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news