SOKO KUBWA SANA CHINA: Kulima tukipania, tutapata pesa sana,Ni maharage ya soya, Fursa nzuri

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

SERIKALI ya Tanzania ni miongoni mwa nchi za Dunia hii ambayo imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo maliasili, ardhi yenye rutuba, madini na nyinginezo ambazo zikitumika ipasavyo itaondokana na tatizo la umaskini.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki alipokuwa akizungumzia fursa za kibiashara zinazoweza kupatikana nchini China na kuinua hali ya uchumi kwa wananchi wa Tanzania.

Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na mahitaji makubwa ya maharage ya soya, nchini humo yana mahitaji makubwa kwa mwaka.

Balozi Kairuki anaainisha kuwa, kwa mwaka Wachina wanahitaji tani milioni 100 za maharage hayo ambapo wao wanazalisha asilimia 20 tu ya kiasi wanachotumia.

Hii inamaanisha kuwa, asilimia 80 ambayo ni zaidi ya tani milioni 80 za maharage ya soya zinaagizwa kutoka nje. Hii inaashiria kuwa, China ina soko kubwa la maharage ya soya.

Mshairi wa kisasa,Bw.Lwaga Mwambande amekaa chini na kutafakari ukubwa wa mahitaji ya maharage ya soya nchini China na namna ambavyo huko kuna soko kubwa,akaona ni bora awakumbushe Watanzania wenzake namna ambavyo wawanaweza kuitumia fursa hiyo watakaupa kisogo umaskini kupitia kilimo cha maharage hayo ambayo pia mahitaji yake ni makubwa hapa nchini. Hatua kwa hatua fuatilia hapa chini ujifunze jambo. Karibu;
NI soko la uhakika, maharage soya China,
Hapa tukichakarika, kilimo bidii sana,
Pesa nyingi tutanyaka, za hapa na huko china,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

TANI milioni mia, wanazohitaji China,
Vizuri ni Tanzania, twaweza kuuza china,
Kulima tukipania, tutapata pesa sana,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

BALOZI katuambia, ni yule wa kwetu China,
Kilimo kukazania, itakuwa vema sana,
Uwezeshaji wa nia, kulipata soko China,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

ARDHI ya Tanzania, kwa kilimo nzuri sana,
Yaweza kutupatia, tani zakutosha sana,
China tukaiuzia, kwa bei ya kupatana,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

MIKOA ya Tanzania, ilimayo mingi sana,
Fursa tukitumia, itakuwa vema sana,
Wakulima kuwambia, muda kushughulishana,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

MBEYA Njombe wasikia, fursa mnaiona?
Ruvuma Songwe pitia, ndiyo twatangaziana,
Iringa na Tanga pia, bora kuhamasishana,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

MOROGORO mwasikia, maharage soya China,
Nafasi Rukwa tumia, Katavi muweze ona,
Kigoma mkipatia, pesa nyingi mtavuna,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

KAGERA changamkia, Singida fursa ona,
Hebu tulime kwa nia, kulipata soko China,
Pesa tutajipatia, uchumi ukue sana,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

SOKO ni kugombania, bidhaa kufika China,
Tusije tukatulia, wengine wakaliona,
Tuzidi papatikia, tuuze tukishavuna,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

SISI twakufagilia, Balozi Mbelwa wa China,
Kazi unatufanyia, waupiga mwingi sana,
Kazi twaifurahia, fursa tunaziona,
Ni maharage ya soya, soko kubwa sana China.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments