TUJITOKEZE KUHESABIWA:Ni mwezi wa Agostia, Si mbali imekaribia

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.

Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya Sensa hiyo.
Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Ungana na Dkt.Mohamed Omary Maguo ambaye ni Mshairi wa Kisasa, Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kujifunza jambo kutoka katika shairi lake, utenzi namba moja wa hamasa kwa umma kujitokeza kushiriki Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania;

1:Sensa imeshawadia
Ni mwezi wa Agostia
Si mbali imekaribia
Tutokeze kuhesabiwa

2:Maendeleo kupangilia
Nchini mwetu Tanzania
Sensa itatoa njia
Tutokeze kuhesabiwa

3:Vituo vile vya afia
Zahanati sipitalia
Sensa kiunganishia
Tutokeze kuhesabiwa

4:Wa mijini na vijijia
Sensa ndiyo stratejia
Maendeleo kuinjinia
Tutokeze kuhesabiwa

KUHUSU SENSA

Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.

Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.

Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.

Post a Comment

0 Comments