Tume huru inazungumzika,katiba mpya bado sana asema Bernard Membe

NA AHMAD MMOW

ALIYEWAHIA kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya Awamu ya Nne, Benard Membe amerejea rasmi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kijiji cha Chiponda, Tarafa ya Rondo Wilaya ya Lindi.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka HAMDU Shaka akimkabidhi ya CCM,aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe aliyerejea CCM, katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtama, Nape Nnauye.

Membe ambaye alipokewa rasmi Mei 29, 2022 katika chama hicho tawala na Katibu wa Idara ya Uratibu na Uenezi Taifa, Shaka Hamdu Shaka alisema suala la tume huru ya uchaguzi linazungumzika na kutoa uwezekano wa kuwa na tume hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Aliweka wazi kwamba, tume huru itapunguza malalamiko baada ya uchaguzi. Huku akitamba kwamba watashinda wapinzani kwa ushindi wa kishindo hata kama kutakuwa na tume huru. Kwani kwa tume ya sasa wapinzani wanapata visingizio kila wanaposhindwa kwenye chaguzi.

Kuhusu katiba mpya alisema ili kupata katiba mpya mchakato wake ni mrefu na unatumia muda mwingi. Lakini pia kunahitajika utulivu na umakini mkubwa.

Kwa kuzingatia ukweli huo Membe alisema, anakubaliana na rai ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba jambo hilo linahitaji muda wa kutosha.

Alisema, kwa sasa wanaodai katiba mpya wampe muda Rais Samia ili afanye shughuli ambazo zitawaletea maendeleo na yafanyike marekebisho katika katiba ya sasa.

Akizungumzia hali ya siasa nchini, kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi alisema Rais Samia amerejesha mshikakamano na kusababisha wananchi wajione ni wamoja.

Lakini pia alisema Rais Samia ameifanya nchi isionekane kama kisiwa mbele ya mataifa mengine duniani. Kwani amerejesha mahusiano na mataifa mengi duniani.

Aidha, mwanadiplomasia huyo aliweka wazi kwamba juhudi zinazofanywa na Rais zitatoa matokeo chanya. ikiwamo idadi ya wawekezaji na watalii kuongezeka.

Alizitaja baadhi ya sababu za yeye kuamua kurejea CCM kuwa ni kutekeleza ushauri na rai ya viongozi wa dini, hasa waislam na wakristo ambazo alitaja kuwa ni dini kubwa hapa nchini, wanasiasa wa ngazi ya kitaifa na mikoa, marafiki na wana CCM ambao wote walimshauri na kumrai arejee CCM.

Aliitaja sababu nyingine kuwa ni kilichomuondoa CCM sasa hakipo. Kwa hiyo kwa kuzingatia ukweli huo ameamua kurudi kwenye chama kilichomlea, kumtunza na kumsomesha.

Alimshukuru Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM taifa kwa kumkutanisha na wajumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu kuu ambao baada ya kumsikia maelezo yake waliliridhia arejee kwenye chama hicho tawala.

"Nilipo ondolewa ndani ya CCM nilisikitika na kusononeka sana. Sasa nimerudi na sitahama tena, nitakitumikia chama changu hadi mwisho wa uhai wangu. Na sababu zilizosababisha nihame zimekwisha,"alisisitiza Membe.

Kwa upande wake katibu wa idara ya itikadi na uenezi taifa, Shaka Hamdu Shaka alisema Membe na wenzake 1,670 ambao wamerejea CCM watapewa kadi kwenye matawi yao. Kwani wamekidhi matakwa na vigezo vilivyopo kwenye katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Benard Membe na wenzake 1,670 walihama kutoka CCM na kujiunga na ACT- Wazalendo mwaka 2020 hali iliyosababisha mgombea wa udiwani katika kata ya Chiponda kupitia ACT- Wazalendo kushinda kiti hicho.

Diwani ambaye anaendelea kushika wadhifa huo wa uongozi wa umma katika kata hiyo ambayo ni nyumbani kwa Membe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news