Ustawi wa demokrasia,utawala bora,uhuru wa habari wampaisha Rais Samia anga za Kimataifa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametajwa na jarida la TIME 100 kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Mkuu wa Majeshi (CDF) Venance Mabeyo mara baada ya kufungua mkutano Mkuu wa tano wa Makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliofanyika mwaka 2021Lugalo jijini Dar es Salaam. (Picha na Maktaba/Ikulu).

TIME 100 limemtaja Rais Samia katika orodha hiyo kutokana na uongozi wake wa kusisimua tangu alipoingia madarakani Machi, 2021 na kuleta mabadiliko makubwa kwa Tanzania ikiwemo kufungua mlango wa mazungumzo kati ya wapinzani wa kisiasa nchini.

Jarida hilo limesema, hatua hizo zimechukuliwa ili kujenga upya imani katika mfumo wa kidemokrasia, juhudi za kuongeza uhuru wa vyombo vya habari na amekuwa mfano wa kuigwa na wanawake na wasichana wengi.

Rais Samia ameungana na marais kutoka nchi nyingine katika orodha hiyo wakiwemo Volodymir Zelenskyy wa Ukraine, Xi Jinping wa China, Vladimir Putin wa Urusi na Joe Biden wa Marekani.

Akimzungumzia Rais Samia kupitia jarida hilo, Rais mstaafu wa Liberia, Hellen Johnson Sirleaf, amesema Rais Samia aliyeingia madarakani Machi, 2021 na utawala wake umekuwa wa nguvu.

“Mlango umefunguliwa kwa majadiliano kati ya mahasimu wa kisiasa, hatua kadhaa zimechukuliwa kujenga imani katika mfumo wa demokrasia, hatua zimechukuliwa kuongeza uhuru wa habari na wanawake na wasichana wanaye mtu wa mfano, Septemba 2021, ikiwa ni miezi michache tangu aingie madarakani, Samia alitoa hotuba yenye mwelekeo kama kiongozi wa Awamu ya Sita mwanamke wa Afrika alipohutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,”amesema.

Aidha, Sirleaf ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel alisema Samia alisimama katika eneo alilosimama yeye miaka 15 iliyopita kama mwanamke wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia Afrika.

Post a Comment

0 Comments