Wazazi wafanya 'surprise' Shule ya Sekondari Kata ya Mwandet

NA DIRAMAKINI

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari Mwandet mkoani Arusha wamenunua basi dogo la abiria, ili kuwasaidia walimu wa shule hiyo na kuwapunguzia adha ya usafiri.
Shule ya Sekondari Mwandet ipo katika Kata ya Mwandet wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha. Jina la shule limebeba jina la kata nzima yenye vijiji vinne ikiwemo Losikito, Engutoto, Engalaoni na Imbibia.

Aidha, shule ipo katika Kijiji cha Imbibia ikiwa imezungukwa na jamii ya Kimasai hivyo kuwa katika mazingira rafiki ya kusoma bila kuchangamana sana na tamaduni za mijini.

Uamuzi huo umetokana na walimu hao kufanya kazi kubwa ya kuzalisha rasilimali watu na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Wakizungumza shuleni hapo, baada ya kununua gari hilo, baadhi ya wazazi hao walisema hatua yao ni kama shukrani kwa kile wanachofanya walimu hao.

Mzazi Lotegerwaki Merusori amesema, gari hilo pia litasaidia walimu hao kwani baadhi walikuwa wakitembea umbali mrefu kutoka wanakoishi ili kufika shuleni.
Naye Loivy Ngailova amesema, walimu wanawafundishia watoto wao vizuri na wanafaulu, hivyo hawana budi kuwashukuru kwa kuwapunguzia baadhi ya changamoto.

"Shule ya Mwandet inakabiliwa na changamoto ya nyumba za walimu, kutokana huduma wanayotoa na kutoa matokeo chanya kwa watoto wetu, tumeamua kununua gari hili, liwasaidie usafiri, "amesema Ngailova.

Naye Mkuu wa shule hiyo, John Massawe amesema, wazazi na jamii waliyafurahia matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne na sita, hali iliyofanya kununua gari kama sehemu ya kuwashukuru walimu, kwani wanakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu zilizopo ni tisa, wakati mahitaji ni 51.

Amesema baada ya wazazi kuona changamoto hiyo, wakatafakari hata wakijenga nyumba moja itamnufaisha mwalimu mmoja, hivyo wakaona wanunue usafiri utakaowanufaisha walimu na wanafunzi kwa pamoja.

"Tuna uhaba wa nyumba za walimu shuleni hapa, ikiwa wengi wao huishi mbali na shule kutokana na wazazi wao wenyewe kuweka ahadi juu yetu kwamba tukiondoa ziro shuleni kwetu watatufanyia kitu kikubwa.

“Hivyo tunawashukuru wazazi hao kwa kutimiza ahadi yao kwetu na sisi tunawaahidi tutafanya kazi kweli kweli,"amesema Massawe.
Shule hiyo ipo umbali wa kilomita 12 kutoka katika mji mdogo wa Ngaramtoni na ina kidato cha kwanza mpaka cha sita huku ikiwakutanisha pamoja wanafunzi wanaotoka maeneo mbalimbali hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news