Wazee rudini kwenye kundi tuwasaidie vijana watoboe asema Prof.Hoseah baada ya kuibuka kidedea urais TLS tena

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS),Profesa Edward Hoseah ameendelea kukitetea kiti chake cha urais kwa kuibuka mshindi kwa kupata kura 621.

Akitangaza matokeo hayo jijini Arusha leo Mei 27,2022 katika ukumbi wa mikutano wa AICC, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Charles Rwechungura amesema kuwa, kura zilizopigwa zilikuwa 1,150 ambapo Profesa Hoseah ameibuka mshindi dhidi ya wagombea wenzake ambao ni Harold Sungusia (380) na Jeremiah Mtobesya (145).
Rais mteule wa TLS, Prof.Edward Hoseah ambaye anatarajia kuapishwa kesho.

Profesa Hoseah amemshukuru Mungu kwa kumtetea katika nafasi hiyo huku akiwashukuru wanachama hao kwa kumwamini na kumchagua tena kuwaongoza kwa mara ya pili.

"Mimi niseme tu sasa kwa kuwa mmenichagua tuache kutegemea wanachama kutoa hela zao, na natanguliza kuwepo kwa uwazi kwenye swala la hesabu tutakuwa makini Sana katika maswala hayo na nawaahidi katika hilo," amesema Prof.Hoseah.

Amesema kuwa, atahakikisha kila kamati inawajibika kwa wanachama wake, huku akiwataka kuwa kitu kimoja.

"Wazee rudini kwenye kundi tuwasaidie vijana watoboe na nawaomba vijana mtumie mazingira yaliyopo kwenye nchi yetu ili tuweze kuwekeza wao kama wanasheria na waache kulialia kwani muda umefika sasa wa kutoboa," amesema.

Post a Comment

0 Comments