Waziri Bashungwa:Tufanye maamuzi ya haraka katika nafasi za kukaimu

NA OR -TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaelekeza Katibu Mkuu, Utumishi na OR-TAMISEMI kufanya maamuzi katika nafasi wanazokaimu Maofisa Utumishi nchini.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo Mei 27, 2022 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, lengo likiwa kuwakumbushwa wajibu wao katika uwajibikaji kazini, uadilifu na ubunifu katika kazi.

Amesema, bado kuna Maofisa Utumishi ambao wamekaimu nafasi hizo kwa muda mrefu na kwamba kama wana sifa zinazohitajika ni vyema kuthibitishwa ili kuongeza ufanisi kwenye majukumu yao.

"Nafasi za kukaimu kwa muda mrefu zinaweza kusababisha uzorotoshaji wa kazi kwa kutoheshimiana, kudharauliana hata kusababisha kutokutoa huduma bora kwa wananchi,"amesema. 

Kutokana na hali hiyo, Waziri Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu, Utumishi Dkt.Laurean Ndumbaro na Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe kulifanyia maamuzi ya haraka kwa maafisa waliokaimu kwa muda mrefu wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ili kama wanasifa ya uteuzi kwa nafasi husika.

"Mtumishi mwenye uteuzi wa nafasi yake moja kwa moja ni dhahiri tutaongeza uwajibikaji, heshima na ufanisi katika kazi," amesema Mhe.Bashungwa.

Aidha, amewaelekeza baadhi ya maafisa utumishi kuacha kutoa lugha zisizo kuwa na ari kwa watumishi wenzao kufanya kazi kwani usimamizi wa rasilimaliwatu unaendana na uzalishaji wa uchumi wa nchi na hii inaendana na shabaha ya Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

"Kila mtumishi ana wajibu wa kusikilizwa, kwa sababu kila mmoja ana mchango wake kwa Taifa tushirikiane katika kuhakikisha tunafanya kazi Kwa kufuata taratibu za kazi, lakini pia Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imeaminika kwa ajili ya kusimamia wananchi na Serikali, hii ndio inayotekeleza Ilani ya chama kwa kuhakikisha inatoa huduma bora kwa waliotuamini ambao ni wananchi wenzetu," amesema Mhe. Bashungwa,

Post a Comment

0 Comments