Yanga yakanyagia gia, MO Dewji asema kituo kinachofuata ni maamuzi magumu Simba SC

NA GODFREY NNKO

MWEKEZAJI pekee kwa umiliki wa asilimia 49 ya hisa zenye thamani ya Sh. Bilioni 20 katika Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara bilionea Mohamed Dewji (Mo Dewji) licha ya kuwapongeza watani wao, Yanga SC kwa kuendelea kuupiga mwingi ameonekana kuumizwa na mwenendo mbovu wa klabu yake.
Simba kwa sasa imeonekana kutokuwa na maajabu ya kutisha wakiwa dimbani ambapo katika mtanange wa leo, safu yao ya mbele imeonekana dhaifu.

"Hongereni watani. Huu umekuwa msimu mbaya zaidi kwa Simba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Bodi inahitaji kufanya maamuzi magumu ili iweze kusonga mbele.

"Tunahitaji kurekebisha timu na mkakati wetu wa kurudi kwenye mstari. Tumekosa ari, ari na njaa ya kushinda vikombe mwaka huu,"ameeleza Mo Dewji.
Kilichowapata

Katika dakika 90 za mchezo huo wa Watani wa jadi, Yanga na Simba zimemalizika kwa timu ya Yanga kuitwanga Simba SC bao 1-0 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa watani wa jadi kutoana jasho zilikamilika na ubao ukiwa unasoma Yanga 1-0 Simba.

Dakika 15 za mwanzo ilikuwa ni msako kwa kila timu kutafuta bao la kuongoza ambapo hakukuwa na aliyeweza kuona lango la mpinzani.

Yanga ilibidi wasubiri mpaka dakika ya 25 huku mtupiaji akiwa ni Feisal Salum kwa shuti kali akiwa nje ya 18 likamshinda mlinda mlango namba mbili wa Simba, Beno Kakolanya.

Sasa Yanga inakwenda fainali itakutana na mshindi wa mchezo kati ya Coastal Union ama Azam FC ambao utachezwa kesho.

Post a Comment

0 Comments