CAG avitaka vyombo vya habari nchini kujikita katika habari za uchunguzi,awaeleza Wahariri mambo muhimu

NA GODFREY NNKO

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), CPA Charles Kichere amevitaka vyombo vya habari nchini kujikita katika uandishi wa habari za uchunguzi (Investigative Journalism) ili kuwezesha kulinda rasilimali za umma kwa manufaa ya nchi.

Amesema, vipo vyombo vya habari vichache hasa magazeti ambayo yamejikita kuandika habari za uchunguzi na kwamba yanafanya vizuri sana katika kuandika habari za uchunguzi ambazo zina tija kwa taifa.
Ameyasema hayo leo Mei 28,2022 wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Saalaam, ambapo pamoja na mambo mengine amevipongeza vyombo vya habari kwa kuendelea kufanya kazi nzuri kwa kutumia kalamu zao kufikisha habari za ripoti za ukaguzi kwa wananchi na wadau wengine.

"Vyombo vya habari yakiwemo magazeti, radio, televisheni, mitandao ya kijamii na kadhalika vimekuwa vikiwafahamisha wananchi kwa mapana na marefu juu ya yaliyomo kwenye ripoti hizo mara baada ya kuwasilishwa bungeni. Kwa kweli ushirikiano wenu umekuwa ni chachu ya ripoti za CAG kufahamika kwa wananchi na wadau wengine majukumu mliyobeba yana thamani sana kwetu na tunawashukuru sana kwa hilo," amesema CAG Kichere.

Ameongeza kuwa, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari ameamua kukutana na Wahariri ili kuwafafanulia masuala mbalimbali yanayohusiana na ukaguzi katika kuwajengea uelewa mpana zaidi wa kutambua mambo mbalimbali na shughuli zinazofanywa na Ofisi ya CAG, majukumu yake kikatiba, mamlaka pamoja na ripoti wanazozitoa.
"Ni katika kuchagiza mahitaji ya uwazi na uwajibikaji katika shughuli za Serikali katika kuelimisha jamii juu ya masuala ambayo yana tija kwa nchi yetu. “Hivyo huu si mkutano wa kawaida bali ni mkutano wenye lengo mahususi la kuwajengea uwezo ninyi Wahariri wa vyombo vya habari kuwa na uelewa juu mamlaka niliyonayo, majukumu niliyopewa kikatiba pamoja na ripoti mnazotoa.

"Mihimili mitatu ya dola kwa maana ya Serikali, Bunge na Mahakama ambayo ina majukumu yake mahususi kwa kila mhimili kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu na sheria zetu tulizonazo.Lakini kama ambavyo imekuwa imesemwa na kufahamika kwa wengi vyombo vya habari ni mhimili usio rasmi na unaitwa mhimili wa nne,” amesema.

Ameongeza kuwa, vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa na nafasi ya kimkakati katika jamii kutokana na kuweza kuitazama mihimili mingine ya dola na kama inakwenda kinyume huweza kupaza sauti na vyombo vya habari haviwezi kupuuzwa hata kidogo kutokana na umuhimu wake katika utawala bora, uwazi na uwajibikaji.
Amesema, taarifa ambazo huandikwa na vyombo vya habari zimekuwa zikisaidia katika masuala yenye usimamizi wa rasilimali za umma na katika Ofisi ya CAG na taasisi zingine.

CAG amebainisha kuwa,katika ofisi hiyo kuna utaratibu kila siku ambao umewekwa wa kufuatilia kila kilichoandikwa kwenye vyombo vya habari ili kubaini habari zilizoandikwa kuhusiana na rasilimali za umma na kwamba wanapoona habari imeandikwa hatua huchukuliwa kwa lengo la kusaidia kupata maeneo hatarishi kwenye usimamizi wa rasilimali za umma na kuandaa mpango kazi wa ukaguzi katika maeneo hayo.
Amesema, wanapoona habari zimeandikwa katika vyombo vya habari wamekuwa wakichumua hatua kwani taarifa hizo ni muhimu sana katika kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa kwa manufaa endelevu huku akiwaomba wanahabari kuendelea kuandika habari hizo, kwani ni wadau muhimu sana katika kusaidia rasilimali za umma ziwe na tija kwa taifa.

Akijibu maswali kuhusu sheria ya manununuzi amesema, imekuwa na changamoto kubwa na mapungufu kadhaa ambayo yanafanyiwa kazi na Serikali.

CPA Kichere amesema, sheria hiyo inatakiwa kufanyiwa mabadiliko ili kuisaidia Serikali huku akisisitiza kuwa, wasimamizi wa sheria hizo wanatakiwa kuwa waadilifu ili kazi isonge mbele.

Wakati huo huo akielezea kuhusu suala la mazingira amesema, kuna kila sababu ya kuongeza nguvu katika eneo hilo na akakiomba Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuwa ofisi ya CAG itaongeza kasi ya ukaguzi vinginevyo nchi itageuka kuwa jangwa.

Katika hatua nyingine CAG Kichere akijibu suala la vitisho amesema ofisi yake haiogopi vitisho vya mtu yeyote, kwani wanafanya kazi kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria.

Pia wapo kwa ajili ya kufanya kazi za Serikali na kuangalia maslahi ya Taifa na wananchi na kuwa wamekuwa na ushirikiano mzuri dhidi yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasa katika eneo la manunuzi.
Katika hatua nyingine, wakati wadau mbalimbali hapa nchini wakitaka watumishi wa umma wanaohusika na ubadhirifu wawajibishwe, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), CPA Charles Kichere amesema, baadhi ya taarifa za ripoti za ukaguzi alioufanya zimechukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya kuzifanyia kazi.

Pia, CAG Kichere ameshauri Sheria ya Manunuzi ya Umma ifanyiwe marekebisho ili kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na kusababisha fedha za umma kufujwa.

Amesema, sheria ya manunuzi ya umma inatoa mwanya wa fedha za umma kufujwa na watendaji wasio waaminifu kupitia ununuzi wa vitu mbalimbali kupitia zabuni wanazozitangaza.

“Unakuta kitu sokoni kinauzwa shilingi 1,500 lakini watu wamenunua kwa shilingi 5,000 na unapofuatilia unaona wamekidhi matakwa na wamefuata sheria na taratibu zinazotakiwa...kuna haja ya kuifanyia marekebisho sheria ya ununuzi ili kunusuru fedha za umma,”amesema.

"Kenya wameshafanya mabadiliko ya sheria kama hiyo, akisema ofisi ya CAG inajielekeza katika thamani halisi ya kitu kilichonunuliwa".

Hivi karibuni changamoto kama hiyo imejitokeza katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambapo ripoti za CAG zilibainisha vifaa vilivyonunuliwa kwa bei kubwa tofauti na uhalisia.

Mei 5, 2022 akiwa mkoani Arusha, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliiagiza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB) kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika na ubadhirifu kwenye manunuzi ya vifaa vya afya katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambavyo vilipaswa kununuliwa kwa fedha za Uviko-19.

Alisema MSD walitakiwa kununua kipimo cha sukari ambacho kwa bei ya kawaida ni Sh150 lakini walinunua kwa Sh300, kipimo cha mkojo bei ya kawaida Sh200 kimoja lakini wakanunua kwa zabuni Sh780, walikuwa wananunua kipimo kidogo cha hamolojia ya mwili kinauzwa Sh2,100 wao wakununua kwa bei ya zabuni Sh4,500.

Pia Aprili mwaka huu, CPA Kichere aliwasilisha ripoti ya ukaguzi wa shughuli za Serikali, mifumo ya udhibiti wa ndani na taarifa za fedha kwa mwaka wa fedha 2020/21, kuanzia Julai 1, 2020 hadi Juni 30, 2021.
Katika ripoti hiyo, CAG alibaini ubadhirifu katika taasisi mbalimbali, ikiwemo uwepo wa madai ya bima ya afya yaliyohusisha wanaume 56 waliodaiwa kupata huduma ya upasuaji wa kujifungua na wengine kujifungua kwa njia ya kawaida, ni miongoni mwa mambo yaliyobainika katika ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30, 2021.

Mbali na hayo, katika ripoti hiyo iligundulika kuwa mashine 89 za makusanyo ya faini za makosa ya usalama barabarani zinazotumiwa na trafiki hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo wa malipo wa Serikali.

Katika mkutano wake wa jana, Kichere alipata fursa ya kutoa mada na kujibu maswali ya wahariri ambapo baadhi ya wahariri, wakiwemo Joseph Kulangwa na Salim Said Salim walimuuliza Kichere anajisikiaje mapendekezo ya ripoti zake kutofanyiwa kazi

Katika majibu yake, Kichere alisema kila mkaguzi anapenda kuona ripoti, maoni na mapendekezo anayoyatoa yanafanyiwa kazi ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza zisijirudie katika kaguzi zijazo.

Kichere pia alisema tatizo jingine ambalo analiona ni baadhi ya fedha za Serikali kutumiwa bila kupita katika mfuko mkuu (hazina) ambao yeye ndiyo anaidhinisha.

“Hili jambo lilionekana sana, inaonekana fedha nyingi ni zile za miradi zinazotoka kwa wafadhili na kwenda moja kwa moja kwenye miradi husika,” alisema.

Kuhusu gawio

Kichere alisema baadhi ya mashirika ya umma yalitoa gawi kwa Serikali, lakini kwake fedha walizotoa walisema ni mchango.

“Gawio haliwezi kutolewa na shirika linalopata hasara, hivyo wale waliosema wametoa gawio ama walikosea au walifanya hivyo kwa makusudi,” alisema.

Katika mkutano huo, Kichere alisema vyombo vya habari ni wadau muhimu na vina mchango mkubwa katika kuimarisha utawala bora na kuchagiza mahitaji ya uwazi katika shughuli za Serikali kwa kuelimisha jamii kwenye masuala yenye tija kwa Taifa.

Alivishukuru vyombo vya habari namna vinavyotekeleza majukumu yake kufikisha taarifa za ripoti za ukaguzi unaofanywa na ofisi yake. Alisema ameshuhudia namna ambavyo vyombo vya habari vinatoa ufafanuzi wa ripoti za CAG baada ya kuwasilishwa Bungeni.

“Taarifa zenu huwa tunazotumia kupata maeneo hatarishi katika suala la usimamizi wa rasilimali za umma kisha kuandaa mpangokazi na ukaguzi katika eneo hilo,” alisema Kichere.

Akizungumza kwa niaba TEF, Salim Said Salim alisema Ofisi ya CAG imefanya jambo jema kuandaa mkutano huo uliowaongezea uelewa wahariri na waandishi hivyo akataka ushirikiako huo uboreshwe zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news