Benki Kuu yatangaza Kanuni za Fedha za Kigeni za Mwaka 2022

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga amesema kuwa, tayari Kanuni mpya za Fedha za Kigeni za mwaka 2022 zimetungwa.

Ameyaeleza hayo leo Juni 8, 2022 kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma ikielezea kuhusina na Kanuni za Fedha za Kigeni za Mwaka 2022.

"Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuufahamisha umma kuwa Kanuni mpya za Fedha za Kigeni za mwaka 2022, zimetungwa chini ya Sheria ya Fedha za Kigeni, Sura ya 271 kupitia Tangazo la Serikali Na. 294, lililochapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 13 Mei 2022.

"Pamoja na mambo mengine, Kanuni hizo zinaruhusu wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, kuwekeza katika dhamana za Serikali za muda mfupi na mrefu. Aidha, Kanuni hizo zinaruhusu mkazi wa Tanzania kuwekeza katika nchi wanachama wa jumuiya hizo.

"Hivyo, Kanuni za Fedha za Kigeni za mwaka 2022 zimefuta Kanuni za Fedha za Kigeni za mwaka 1998 na Kanuni za Fedha za Kigeni (Dhamana zilizoorodheshwa katika soko la Hisa) za mwaka 2003. Kanuni za Fedha za Kigeni za mwaka 2022 zinapatikana katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania www.bot.go.tz,"ameeleza Prof. Florens Luoga,Gavana Benki Kuu ya Tanzania.

Post a Comment

0 Comments