HGWT:Mara tuendelee kuwathamini, kuwalinda na kuwasaidia watoto

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara limetoa rai kwa jamii kuendelea kuwathamini, kuwalinda na kuwasaidia watoto kwa kuwapa mahitaji yao kwa manufaa endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla. 
Kauli hiyo imetolewa Juni 16, 2022 na Mkuu wa Kituo cha 'Hope Mugumu Nyumba Salama' kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Daniel Misoji wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambapo katika Wilaya ya Serengeti yamefanyika katika Shule ya Sekondari Makundusi iliyopo wilayani humo. 

Misoji amesema kuwa, Kila mwanajamii anapaswa kushiriki katika jukumu zima la ulinzi na usalama wa mtoto pamoja na kuhakikisha kwamba mila kandamizi dhidi ya Watoto zinakomeshwa ili Watoto wazidi kukua katika Ustawi bora pamoja na kuhakikisha haki zao zinalindwa na kuheshimiwa. 

"Tunapoadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika niombe Watoto walindwe, hasa Watoto wa kike ambao kwa kiasi kikubwa hufanyiwa ukatili katika Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara niombe jamii inayokeketa iache ukeketaji, una madhara makubwa kwa watoto wa kike. Watoto wa kike wasomeshwe, wapatiwe mahitaji yao ya msingi na kuthaminiwa kwani ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima,"amesema Misoji.
"Ukimkeketa mtoto wa kike tambua unamuathiri kisaikolojia, unamuondoa kujiamini, unamwandaa kumuoza, unamfanya awe katika hatari ya kupoteza maisha kwa kutokwa damu nyingi, kupata kovu la kudumu ambalo kwa baadaye ni hatari kwa maisha yake wakati wa kujifunza na pia ni chanzo Cha magonjwa ya kuambukiza," amesema Misoji.

"Tuachane na mila mbaya ambazo hazina faida kwa masilahi ya Jamii na taifa, natambua mwaka huu unagawika kwa mbili hivyo Kuna koo zimejipanga kukeketa niombe zisifanye hivyo. Bali nguvu iwe katika kuwasomesha Watoto wa kike na siyo kuwatendea ukatili. tuwalee pia Watoto waote katika misingi ya kumuabudu Mungu na kuwafundisha maadili mema na mila nzuri zenye manufaa katika jamii. Kwa kumpenda mtoto utamlinda, utamsikiliza, mtamheshimu na kumtimizia haki na mahitaji yake yote,"amesema Misoji.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti,Cosmas Kamara akizungumza katika maadhimisho hayo ameitaka jamii kutambua kwamba ukatili dhidi ya mtoto ni kosa kisheria na kwamba amesema Serikali Wilayani Serengeti haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kufanya vitendo vya ukatili dhidi yao. 

Pia, Kamara amesema kuwa serikali Wilayani humo imejipanga kuchukua hatua kali za kisheria kwa wazazi waliojipanga kuwakeketa Watoto wao. Ambapo amesisitiza Jamii na kila mmoja kushiriki kuwalinda Watoto wa kike na kwamba wasiwafumbie macho kuwafichua mbele ya vyombo vya sheria wataofanya vitendo hivyo ambavyo vinakiuka haki na Katiba ya nchi. 

Aidha, ametoa msisitizo kwa Wazazi na walezi kuwasomesha Watoto wa kike na kushiriki katika kuwawezesha wafikie ndoto zao, na kwamba mchango wao ni muhimu kwa Maendeleo ya Jamii na taifa iwapo wakiandaliwa vyema bila kukwamishwa ndoto zao. 

Juma Petro na Agnes Richard ni wakazi wa Makundusi wakizungumza na DIRAMAKINI wamesema, jukumu la ulinzi na usalama wa watoto linapaswa lianzie ngazi ya familia hasa wazazi kuwapenda watoto na kuwafundisha tabia njema ambazo zinatija kwa jamii.
"Watoto wafundishwe adabu, nidhamu, mila nzuri, na kila mmona aone kwamba mtoto wa mwenzake ni mtoto wake kwa hiyo akiona anakengeuka au anafanya mambo yasiyofaa akemewe na kuwekwa katika mstari unaofaa,"amesema Agnes Richard.

Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly kwa kushirikiana na Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia na Watoto (Polisi) walizifikia Shule 48 za Msingi wilayani humo wakitoa elimu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kuunda klabu za wanafunzi wa kupinga vitendo hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news