Hureeeeeeeeeeeee Serengeti Girls, asanteni kwa Kufuzu Kombe la Dunia

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake U-17 (Serengeti Girls) imefanikiwa kufuzu Kombe la Dunia baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cameroon mchezo uliochezwa jioni ya leo kwenye dimba la Amaan jijini Zanzibar.
Bao pekee la Serengeti Girls limefungwa na Neema Paul dakika 47 na kuifanya Tanzania itinge Kombe la Dunia litakalochezwa Oktoba, mwaka huu nchini India kwa jumla ya mabao 5-1, kufuatia mchezo wa awali kushinda 4-1 ugenini.

Jana kaka zao, wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wametoa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, wahamaji Niger Uwanja wa L'Amitié jijini Cotonou nchini Benin katika mchezo wa kwanza wa Kundi F kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Ivory Coast.

Tafa Stars ilitangulia kwa bao la mshambuliaji George Mpole wa Geita Gold nyumbani dakika ya kwanza tu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Naim-Nhour Jan Van Attenhoven kufuatia krosi ya winga wa Wydad Athletic ya Morocco, Simon Msuva.

Aidha, mshambuliaji wa Isloch ya Belarus, Daniel Sosah akaisawazishia Niger dakika ya 26 akimalizia pasi ya beki wa Monastir ya Tunisia, Youssouf Oumarou Alio.

Mechi nyingine ya kundi F, wenyeji Algeria waliichapa Uganda 2-0, mabao ya A. Mandi dakika ya 28 na Y. Belaïli dakika ya 80 Uwanja wa Julai 5, 1962 jijini Algiers.

Hata hivyo, mechi zijazo, Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Algeria jijini Dar es Salaam na The Cranes watawakaribisha Niger jijini Kampala nchini Uganda.Habari

Post a Comment

0 Comments