KAGERA SUGAR,TIBA YA UTEGEMEZI: Mazingira Tanzania, kuwekeza ni vizuri sana

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

JUNI 9, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akiwa katika siku ya pili ya ziara ya kikazi mkoani Kagera, amezindua Awamu ya Tatu ya Upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar.
Sambamba na Kituo cha kupoza umeme Megawati 20 zitakazotumika kiwandani hapo huko wilayani Missenyi mkoani humo.

Hatua hiyo inalenga kukiongezea uwezo na ufanisi wa uzalishaji wa sukari,kiwanda hicho cha pekee cha sukari katika Kanda ya Ziwa ambacho kinatoa ajira zaidi ya 5,000.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeamua kuendeleza ajenda ya viwanda kwa kasi na mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yameendelea kuboreshwa hivyo kuwapa fursa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika miradi mbalimbali.

Akiwa kiwandani hapo Mheshimiwa Rais amewataka wawekezaji katika viwanda vya sukari nchini kuchangia kikamilifu kufanikisha malengo ya kujitosheleza huku akitaka tufikie ziada ya kuuza nchi za nje ifikapo 2025.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali imeazimia kufanya mageuzi ya kilimo cha kisasa ambayo yanapaswa kwenda sambamba na mahitaji ya viwanda vya ndani ili kuifanya nchi iweze kuwa mzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo Afrika.

Mshairi wa kisasa,Bw.Lwaga Mwambande anakusshirikisha jambo kuhusu kiwanda hicho cha pekee cha sukari Kanda ya Ziwa kupitia shairi lifuatalo, karibu;

1:Tunayo Kagera Sugar, kiwanda chetu kizuri,
Kitendawili natega, tutafikia pazuri,
Sukari nyingi chataga, kwa hakika si kamari,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

2:Viwanda kujivunia, vile ambavyo vizuri,
Nchi inafurahia, uzalishaji mzuri,
Kagera nakutajia, kweli chafanya vizuri,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

3:Nchi yetu Tanzania, tunatumia sukari,
Na tena ninakwambia, hii ichukue siri,
Chai ukijipatia, hiyo ni nzuri habari,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

4:Lakini tupofikia, ni pazuri si pazuri,
Kule kujizalishia, bado tunayo safari,
Mahitaji yazidia, tuzalishayo sukari,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

5:Kagera twashangilia, ni kiwanda cha sukari,
Fursa chaitumia, kutuondolea shari,
Vile kutuzalishia, sukari kama bahari,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

6:Kiwanda nakuambia, kwetu ni njema habari,
Ajira chatupatia, pia mafunzo mazuri,
Vijana Watanzania, wajua kazi vizuri,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

7:Kagera kikichangia, kuizalisha sukari,
Kilombero nao pia, tutengeneze futari,
Pazuri tutafikia, sawa kuwa na mahari,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

8:Kagera Sugar sikia, kwa uchumi ni kizuri,
Kodi nyingi chachangia, za halali si kamari,
Rais kukifikia, jua mambo ni mazuri,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

9:Wawekezaji sikia, wa kiwanda cha sukari,
Kazi yenu twawambia, kwa kweli kwetu ni nzuri,
Sukari tunatumia, na ajira zenu nzuri,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

10:Mazingira Tanzania, kuwekeza ni vizuri,
Ndiyo mambo angalia, Serikali yetu nzuri,
Wengi wanajisikia, kujiunga na safari,
Upanuzi wa kiwanda, tiba ya utegemezi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments