SERIKALI YAWAJALI: Jembe lako mkononi, lima upate manoti

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeazimia kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo cha kisasa nchini.

Mageuzi ambayo yanapaswa kwenda sambamba na mahitaji ya viwanda vya ndani ili kuifanya nchi iweze kuwa mzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo barani Afrika.

Katika kutekeleza mageuzi hayo, Rais Samia akiwa katika siku ya pili ya ziara ya kikazi Juni 9, 2022 mkoani Kagera amesema, Serikali imetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha alizeti na michikichi mkoani humo.

Rais amewataka viongozi wa Mkoa wa Kagera kutenga ardhi kati ya hekari 70,000 hadi laki moja kwa ajili ya kulima mashamba makubwa ya alizeti pamoja na michikichi ili kuondoa utegemezi wa mafuta hayo kutoka nje ya nchi.

Rais Samia Hassan ameyasema hayo wakati akiongea na wafanyakazi katika Kiwanda cha Sukari Kagera kilichopo Wilaya ya Misenyi mkoani humo baada ya kukagua mashamba yanayozalisha miwa.

"Tanzania tumekuwa tukitegemea mafuta ya kula kutoka nje lakini kutokana na janga la UVIKO-19 tumepata tatizo la kukosa mafuta baada ya kufungwa mipaka hivyo hatuna budi kufanya uzalishaji wa ndani na ili tujitosheleze lazima tuwe na mashamba makubwa ya alizeti pamoja na michikichi,"amesema Rais Samia.

Bw.Lwaga Mwambande ambaye ni mshairi wa kisasa anasema kuwa, mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa Tanzania yenye hali nzuri ya hewa, ukiwa na rutuba ya kutosha kuotesha na kustawisha mazao yote, huku ukipata mvua nyingi mara mbili kwa mwaka kuanzia kwa kiwango cha milimita 600 hadi 2000 kwa mwaka. Kwa upekee anakushirikisha taarifa njema kupitia shairi hapa chini, endelea;

1).Bilioni ishirini, hebu lima alizeti,
Pesa hiyo ya shambani, ufanye kujizatiti,
Jembe lako mkononi, lima upate manoti,
Ni fedha za serikali, kuendeleza kilimo.

2).Ni fedha za serikali, kuendeleza kilimo,
Watu wa kila mahali, hilo walipate somo,
Serikali yawajali, kwa vitendo si mdomo,
Michikichi ukipanda, pia utafaidika.

3).Michikichi ukipanda, pia utafaidika,
Mazao haya twapenda, jinsi yanavyotumika,
Kukaangia twashinda, mafuta yanatumika,
Kama tukilima sana, nje hatutaagiza.

4).Kama tukilima sana, nje hatutaagiza,
Tena yana afya sana, tukila twajiongeza,
Kulima ni bora sana, kipato tunaongeza,
Rais ameshasema, kilimo kipaumbele.

5).Rais ameshasema, kilimo kipaumbele,
Kagera zidi kulima, mkoa usonge mbele,
Pesa hizo amesema, kwenu zinakuja tele,
Heko Rais Samia, ziara isonge mbele.

6).Heko Rais Samia, ziara isonge mbele,
Tuzidi sikia mema, tuachane na ukale,
Sote wenye nia njema, tulime kwa kwenda mbele,
Uti wa mgongo wetu, kuimarisha kilimo.

7).Uti wa mgongo wetu, kuimarisha kilimo,
Kufanya juhudi zetu, njaa kwetu isiwemo,
Tupate mazao yetu, kwa wingi bila ukomo,
Tuweze jitosheleza, mengine tuuze nje.

8).Tuweze jitosheleza, mengine tuuze nje,
Maghala tupate jaza, na mengine tuyavunje,
Tupate kuyaongeza, wageni waje waonje,
Jinsi twashikwa mkono, tuzidishe kuzalisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news