M-MAMA KUIFIKIA MIKOA YA LINDI NA MOROGORO

NA OR-TAMISEMI

SERIKALI inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya Mfumo wa Usafirishaji wa Dharura kwa Wanawake Wajawazito na Watoto Wachanga (M-Mama) ambapo ifikapo Julai 2022 mikoa ya Lindi na Morogoro itafikiwa na huduma hiyo.
Huduma yenye lengo la kuepusha vifo vya mama na mtoto kabla,baada na wakati wa kujifungua.

Hayo yamebainishwa leo Juni 9, 2022 katika kikao kazi cha Idara ya Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI pamoja na wadau kutoka Taasisi za Vodafone na Touch ambao wanashirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma ya M-Mama inaifikia mikoa yote 26. 

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Ntuli Kapologwe ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuongeza wigo wa upatikaji wa huduma ya M-mama katika mikoa ya Morogoro na Lindi akisisitiza kuwa huduma hiyo itaimarisha huduma ya mama na mtoto nchini. 
“Niishukuru Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha huduma ya Afya Msingi,nimefurahi kusikia huduma hii kuanzia Julai 2022 itapatikana katika mikoa wa Lindi na Morogoro, ni hatua nzuri,”amesema Dkt. Kapologwe.

Naye Mkurugenzi wa M-Mama kutoka Taasisi ya Vodafone, Dolorosa Duncan amesema kuwa,awali huduma hiyo ililenga kuifikia mikoa 14 tu, lakini kutokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya M-Mama, Serikali kwa kushirikiana na taasisi za Vodafone na Touch itahakikisha huduma hii inapatikana katika mikoa yote 26 ifikapo 2024.

Naye Bi. Linda Deng ambaye ni Mkurugenzi wa M-Mama kutoka Taasisi ya Touch ameiomba Serikali kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na upatikanaji wa mfumo wa huduma ya M-Mama pindi huduma hiyo itapoanza kupatikana katika mikoa husika. 

Huduma ya M-Mama itapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na uhitaji wa matibabu ya dharura, mtoa huduma katika kituo cha afya au mwananchi atapata fursa ya kupiga simu ili mama mjamzito au mtoto mchanga (mwenye umri usiozidi siku 28) aweze kupata huduma ya usafiri ya kupelekwa katika hospitali au kituo cha afya ili kupata huduma ya matibabu zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news