Maagizo ya Rais Dkt.Mwinyi yazigusa idara,taasisi zote nchini

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameziagiza wizara zote za Serikali,mashirika,mikoa,wilaya,manispaa,mabaraza na halmashauri za miji kote nchini kuanza kutumia mfumo wa Ununuzi kwa Njia ya Mtandao (eProcurement) kuanzia sasa. 
Dkt.Mwinyi ametoa wito huo katika uzinduzi wa mfumo wa Ununuzi kwa Njia ya Mtandao (eProcurement), hafla iliofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar. 

Amesema, suala la manunuzi limeghubikwa na urasimu na kuna nyakati shughuli za utekelezaji wa mipango Serikalini huchelewa au kukwama kabisa kwenye vitengo vya manunuzi 

Amesema, pamoja na vitengo vya manunuzi kutakiwa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwazi lakini kumekuwepo na baadhi ya watumishi walioridhika na hali iliopo hivi sasa, hivyo kuibua urasimu, jambo linalowavunja moyo Wazabuni, Wawekezaji na Wafanyabiashara wanaotoa huduma Serikalini. 

Aidha, alibainisha kuwepo baadhi ya viongozi na watendaji wanaojaribu kwa njia za siri kupinga matumizi ya mifumo ya Kielektroniki ili kulinda maslahi yao binafsi. 

“Naagiza kila taasisi yenye jukumu la kufanya manunuzi ihakikishe inatumia mfumo huu katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 unaoanza,”amesema. 

Aidha, Dkt.Mwinyi aliagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria watendaji wa ngazi zote watakaoharibu au kudharau kwa makudusi kutumia mfumo huo. 

Ameeleza kuwa, juhudi za kuunda mifumo zinapaswa kuambatana na utekelezaji wa mikakati imara ya utoaji wa mafunzo kwa watendaji wanaosimamia mifumo hiyo, sambamba na elimu hiyo kutolewa kwa wananchi. 
Amesema, wazabuni na wafanyabiashara wanahitaji kupewa mafunzo ya msingi na kuelimishwa juu ya umuhimu wa kutumia mfumo huo mpya, sambamba na taasisi zinazosimamia utawala bora, hasa Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uhumi Zanzibar (ZAECA) pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufahamu vyema matumizi ya mifumo inayoundwa. 

Alisema mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Mtandao utaondoa urasimu , kuimarisha uwazi, uadilifu pamoja na kuondoa kasoro za uwajibikaji ambazo hutumika kupanua mianya ya rushwa. 

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema kumekuwepo changamoto katika mfumo wa matumizi ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (VFD) , ikihusisha kuwePo wafanyabiashara wanaokataa kutumia mfumo huo kwa makusudi au kukosa elimu juu ya wajibu walionao katika kulipa kodi. 

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Viongozi na Watendaji kushirikiana na Bodi ya Mapato (ZRB) katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya utoaji risiti za Kielektroniki. 

Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema mfumo huo utaleta mafanikio makubwa na kubainisha azma ya Wizara hiyo kuhakikisha hauchezewi. 
Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Sada Mkuya Salum alisema utekelezji wa mfumo huo hautokuwa jambo la hiari, hivyo akaahidi kuusimamia kikamilifu , huku akibainisha kuwepo uadilifu wa kiwango cha chini katika eneo la manunuzi Serikalini. 

Alisema Wizara hiyo inakamilisha taratibu za kubadili sheria ya manunuzi ya mwaka 2011 ili iweze kuendana na wakati uliopo na hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka Viongozi Serikalini kuwa tayari kwa jambo hilo. 

“Hatutopokea manunuzi yoyote baada ya kukamilika kwa mfumo huu kwenda kwenye makaratasi,”alisema. 

Mapema, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Juma Malik Akil alisema lengo la kuandaa mfumo huo ni kuongeza ufanisi na kuwepo usahihi katika mchakato wa manunuzi Serikalini. 

Alisema mashirikiano mazuri yaliopatikana kutoka sekta mbali mbali yamechangia kwa kiasi kikubwa kuandaa mfumo huo, ambao ni bora katika nchi za Afrika Mashariki. 

Alieleza utekelezaji wa mfumo huo utawezesha na kufanikisha dhamira ya Serikali ya kupunguza gharama, muda wa zabuni, kuwepo uwazi na kuleta ufanisi katika zabuni, kutoa huduma bora za kifedha, sambamba na kupunguza wizi na mianya ya rushwa. 

Alisema Ofisi ya Rais Fedha na Mipango inalenga kuzipatia mafunzo Kampuni za ndani ili kupunguza gharama pamoja na kuwepo uwazi katika zabuni.

Katika hatua nyingine, akitoa salam kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Oman Data Park Maqbul Salim Alwaheed alisema mfumo huo si tu kuwa utawezesha kuleta ufanisi katika ukusanyaji na matumzii ya fedha za Serikali, bali utaweka mazingira bora katika masuala mbali mbali, ikiwemo suala la ajira. 

Alisema Oman Data Park inajivunia kuwa miongoni mwa wale waliofanikisha maandalizi ya mfumo huo wenye faida kubwa kwa Serikali na hivyo akatumia fiursa hiyo kuipongeza serikali kwa mashirikiano yake. 
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mansura Mossi Kassim alisema mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Mtandao hautokuwa wa mwisho kuandaliwa, bali kuna mifumo kadhaa inayotarajiwa kushughulikiwa hivi karibuni kwa dhamira ya kuleta ufanisi katika shughuli za serikali, ikiwemo mfumo wa ajira. 

Vile vile Mkurugenzi Mtendaji wa eGovernment Said Seif alisema mafanikio ya kuwepo kwa mfumo huo yatategemea taasisi mbali mbali za serikali pamoja na vitengo vya manunuzi watakavyoupokea na kuutumia. 

Mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Mtandao (eProcurement) umeandaliwa kwa mashirikiano baina ya Viongozi na Wataalamu kutoka Wakala wa serikali Mtandao (eGovernment), Kampuni ya Oman Data Park pamoja na Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news