Ukiuza, ukinunua dai risiti ya kielektroniki ya mkono kataa-Mama Mariam Mwinyi

NA DIRAMAKINI 

MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi ameunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi katika ukusanyaji mapato kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD). 
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi (katikati) akishiriki katika mazoezi ya viungo baada ya mazoezi ya kutembea yaliyoanzia katika Barabara ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini hadi Uwanja wa Amaan leo ikiwa ni utekelezaji wake ya kushiriki mazoezi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa kushirikiana na wananchi (kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe.Idrisa Kitwana Mustafa na Mke wa Waziri Kiongozi Mstaafu, Mama Asha Shamsi Nahodha.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo mara baada ya kumaliza mazoezi yaliyoanza katika Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini hadi uwanja wa Amaan mjini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kufanya mazoezi na wananchi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. 

Ameeleza jinsi anavyofarajika na hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Bodi ya Mapato Zanzibar katika ukusanyaji wa mapato na kueleza jinsi anavyounga mkono juhudi hizo katika kuhamasisha utumiaji wa mashine za kielektroniki (EFD) za kutolea risiti. 

Amewasisitiza wananchi kwamba jambo hilo ni muhimu na wasilifanyie mzaha na kuwasihi kila pale wanapofanya matumizi ni vyema wakadai risiti ya elektroniki (EFD) na wasikubali kupewa risiti iliyoandikwa kwa njia ya mkono. 

Mama Mariam Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF) amesema kuwa, risiti za kielektroniki (EFD) zina faida hata kwa wafanyabishara licha ya baadhi yao kuwa wagumu katika utoaji wa risiti hizo na kuwaeleza kwamba zitawasaidia hata katika kuweka kumbukumbu ambapo pia, ni njia moja wapo ya kuondosha usumbufu. 
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi (katikati) akishiriki katika mazoezi ya Viungo baada ya Mazoezi ya kutembea yaliyoanzia katika Barabara ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini hadi Uwanja wa Amaan leo ikiwa ni utekelezaji wake ya kushiriki mazoezi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kwa kushirikiana na wananchi (kulia) Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Rashid Hadid Rashid.

Aliongeza kwamba, kwa upande wa wananchi kuna umuhmu wa kudai risiti kwani hatua hiyo itasaidia kuhakikisha mapato ya Serikali yanakwenda kama ilivyokusudiwa na kusaidia kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato ya Serikali. 

Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa, mapato yakiongezeka ile safari ya neema tupu ndio inafikiwa na kusisitiza umuhimu wa kudai risiti ili nchi iweze kustawi kwani nchi haiwezi kustawi bila ya kuwa na mapato. 

Aidha, alisema kuwa taasisi ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), imelenga kuwa na masiaha bora kwa wazanzibari na ndio maana imekuwa ikihamashisha jamii kufanya mazoezi hasa ikizingatiwa kwamba mazoezi yanaleta afya bora, umoja, mshikamano, upendo na amani. 
Vikundi mbali mbali vya mazoezi wakifanya mazoezi ya Kunyoosha Viungo baada ya Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi kuongoza Mazoezi hayo leo yaliyoanzia katika Barabara ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini hadi Uwanja wa Amaan leo ikiwa ni utekelezaji wake ya kushirikiana na wananchi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. 

Kwa upande mwengine, Mama Mariam Mwinyi alieleza kuhusu suala zima la usafi na kusema kuwa usafi ni afya kama ilivyo kwa mazoezi kwani usafi unapunguza maradhi katika jamii. 

Aliwasihi wananchi kufanya usafi majumbani huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo maeneo maalum ya kutupa taka na kuweka utaratibu maalum wa kutupa taka hatua ambayo ni vyema ikaanza majumbani na hadi mashuleni. 

Pamoja na hayo, alieleza haja kwa Halmashauri kuweka vifaa na maeneo maalum ya kutupa taka ili kuiweka Zanzibar katika hali ya usafi hasa ikizingatiwa kwamba ni nchi ya visiwa ambapo pia, baadhi ya taka huelekea baharini ambako nako kuna viumbe vya bahari ambavyo huathirika. 

Alisisitiza haja kwa Manispaa kuwepo kwa utaratibu wa kushinda katika kufanya usafi hatua ambayo inaweza kusaidia suala zima la usafi katika jamii hapa nchini. 

Sambamba na hayo, Mama Mariam Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kuhesabiwa na kuwataka wananchi wanajiandaa ipasavyo kwa ajili ya kuhesabiwa siku itakapofika ya Agosi 23, mwaka huu. 

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Leila Mohamed Mussa kwa niaba ya Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo alieleza umuhimu wa mazoezi na kutoa shukurani kwa juhudi za Mama Mariam Mwinyi za kuendeleza utamaduni huo na kuahidi kwamba Wizara hiyo itaendelea kumuunga mkono. 

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa kwa upande wake alimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa kuendeleza mazoezi pamoja na utamaduni wa kutoa ujumbe mara baada ya mazoezi. 

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akiagana na Mke wa Makamo wa Kwanza wa Rais Mama Zainab Othman baada ya kumalizika kwa mazoezi ya Viungo yaliyoshirikisha Vikundi mbali mbali vya mazoezi yaliyoanzia katika Barabara ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini hadi Uwanja wa Amaan leo ikiwa ni utekelezaji wake kushiriki mazoezi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.(Picha na Ikulu).

Alimpongeza kwa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kupitia taasisi yake ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), katika kuwasaidia akina mama, watoto na vijana. 

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali waliungana na Mama Mariam Mwinyi akiwemo mke wa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Othman, Mama Asha Shamsi Nahodha, viongozi wa vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi na vikundi mbali mbali vya mazoezi. 

Mazoezi hayo ni muendelezo wa ahadi yake aliyoitoa mnamo Febuari 19 mwaka huu wakati akizindua taasisi yake ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), ambapo aliahidi atakuwa championi na kinara katika kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kwa kuunganna na wananchi kwa ajili ya kujenga afya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika Wilaya zote za Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments