MAENDELEO KWA WATU: Sote tumemsikia, Rais akitamka,Pesa zitumike vema, bila wajanja

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi mkoani Kagera kusimamia vyema fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Rais Samia ametoa maagizo hayo Juni 8, 2022 wakati akizungumza na wananchi wilayani Biharamulo ikiwa ni katika siku ya kwanza ya ziara ya siku tatu mkoani Kagera.

Amesema kuwa, fedha nyingi zimekusanywa na zitaendelea kuletwa kwa wananchi hivyo hakuna haja ya kukaa nazo au kuona zinatuna kwenye mifuko bure, hivyo ni vyema viongozi walioaminiwa wasimamie vyema miradi mbalimbali ya maendeleo inayotolewa na Serikali kwa malengo husika.

Lwaga Mwambande ambaye ni mshairi wa kisasa kupitia shairi lake licha ya kupongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kutoa kipaumbele kikubwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, anasema agizo la Mheshimiwa Rais si tu kwa viongozi wa Mkoa wa Kagera tu, bali linawahusu viongozi wote nchini, karibu ujifunze jambo hapa;

1:Maendeleo kwa watu, Serikali yapeleka,
Wote waishi kiutu, huduma za kuridhika,
Hilo ndilo lengo letu, Rais ametamka,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

2:Biharamulo kasema, Kagera alipofika,
Kwamba kwa sana ni vema, huduma ziweze fika,
Pesa zitumike vema, bila wajanja kuteka,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

3:Viongozi kaagiza, jambo muhimu kushika,
Fedha za umma chunguza, jinsi zinavyotumika,
Kusiwepo kupunguza, miradi ikaanguka,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

4:Ingawa yuko Kagera, nchi yote yahusika,
Haya matumizi bora, miradi ikifanyika,
Kusitokee hasara, ubadhilifu kufika,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

5:Sote tumemsikia, Rais akitamka,
Tena tunafurahia, miradi kukamilika,
Vile tunaaminia, huduma kuimarika,
Fedha za maendeleo, zitume ipasavyo.

6:Lakini kwenye jamii, vile tumechanganyika,
Kuna wavivu kutii, hivi ameelekeza,
Maonyo hawasikii, kuhujumu wahusika,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

7:Viongozi mkikuta, pesa bure zapunguka,
Hatua msijesita, wahusika kuwashika,
Hukumu wakiipata, pesa watazitapika,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

8:Alivyosema Rais, sote tunafarijika,
Maendeleo ya sisi, viongozi wahusika,
Hivyo mambo yote hasi, watakiwa kuanika,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

9:Vema wakiwajibika, na kazi zikafanyika,
Huduma kuimarika, wananchi kuridhika,
Uhalali wajengeka, wa wao kuaminika,
Fedha za maendeleo, zitumike ipasavyo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news