WIGO WA UWEKEZAJI: Hizi fedha za kigeni, tunazo mpya kanuni,nafasi kwako

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

JUNI 8, 2022 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga amesema kuwa, tayari kanuni mpya za Fedha za Kigeni za mwaka 2022 zimetungwa.

Kanuni ambazo zimetungwa chini ya Sheria ya Fedha za Kigeni, Sura ya 271 kupitia Tangazo la Serikali Na. 294, lililochapishwa katika Gazeti la Serikali la Mei 13, 2022.

Pamoja na mambo mengine,kanuni hizo zinaruhusu wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuwekeza katika dhamana za Serikali za muda mfupi na mrefu na zinaruhusu mkazi wa Tanzania kuwekeza katika nchi wanachama wa jumuiya hizo.

Aidha,Kanuni za Fedha za Kigeni za mwaka 2022 zinapatikana katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ya www.bot.go.tz

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande hatua kwa hatua kupitia ushairi ana jambo la kukushirikisha, lengo likiwa ni kukuwezesha kujifunza kuhusiana na hatua hii muhimu iliyofikiwa na Benki Kuu ya Tanzania.Karibu;

>Hizi fedha za kigeni, tunazo mpya kanuni,
Zimetoka kiwandani, Benki Kuu kule ndani,
Zimewekwa hadharani, kwa matumizi nchini,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Kanuni mpya kabisa, kwa matumizi nchini,
Zinaruhusu kwa sasa, uwekezaji nchini,
Masoko ya fedha hasa, hata wetu majirani,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Hizi Jumuiya zetu, Mashariki na Kusini,
Hao wakazi wenzetu, ruksa hapa nchini,
Masoko ya fedha yetu, kuwekeza kwa amani,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Zinazotajwa SADC, Jumuiya ya Kusini,
Afrika Mashariki, wananchi wote ndani,
Kuwekeza ni mantiki, uchumi bora nchini,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Dhamana za Serikali, zipelekwazo sokoni,
Kwao hao ni halali, kwa kuwekeza sokoni,
Hizi kwetu ni dalili, kushikamana kindani,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Pia upande mwingine, fursa hapa nchini,
Kwa wananchi wengine, kuwekeza ugenini,
Lakini siyo kwingine, Mashariki na Kusini,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka

>Kanuni mpya zafuta, kanuni mbili nchini,
Ambazo ilizikuta, zikitumika sokoni,
Lengo ni watu kupata, kushiriki kwa amani,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Za mwaka tisina nane, Kanuni fedha Kigeni,
Pamoja zile zingine, pia fedha za kigeni,
Hatutaki tuzione, mpya ziko ulingoni,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Elfu mbili na tatu, kanuni fedha kigeni,
Kwa sasa hizo ni kutu, zinakuwa za zamani,
Kwa uwekezaji wetu, hilo jambo la thamani,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

>Shime kwa wawekezaji, kwenye masoko nchini,
Ambao mna mtaji, wa kuingia sokoni,
Kanuni zawahitaji, muingie uwanjani,
Wigo wa uwekezaji, unazidi kupanuka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Post a Comment

0 Comments