MAJI YAFIKE KWA WATU: Ni Kyaka-Bunazi, agizo limeshatoka

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa maji wa Kyaka-Bunazi mkoani Kagera wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Maji Kyaka-Bunazi wilayani Misenyi mkoani Kagera tarehe 9 Juni, 2022. Mhe. Rais Samia anaendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.(Picha na Ikulu).

Uzinduzi huo ameufanya Juni 9, 2022 huku akisema kuwa,mradi huo umejengwa kwa gharama za ndani na umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 15.7 na utanufaisha zaidi ya watu 65,470 wa Kata ya Kyaka na Kasambya pamoja na vitongoji vyake.

Rais Samia ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi pamoja na wahandisi wa mradi huo ambao wengi wao wamefanya sehemu ya pili ya mradi.

Pia ametoa maelekezo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha anazikopesha mamlaka za maji za mkoa huo shilingi milioni 500 ili ziweze kutekeleza miundombinu ya maji kwa wananchi kwa haraka.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anakupitisha hatua kwa hatua katika mradi huo kupitia shairi lifuatalo, jifunze jambo;

>Ni maji Kyaka-Bunazi, agizo limeshatoka,
Watakiwa viongozi, kuhakiki lafanyika,
Watendaji kazikazi, maji kwa watu kufika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Waziri wetu Awesu, ndiye aliyetamka,
Kagera linawahusu, waweze kuwajibika,
Kwa kazi wanoe visu, wazidi kuchakarika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Mradi shazinduliwa, Mama Samia kafika,
Huko ni kufanikiwa, ndoo chini zinashuka,
Muda kuunganishiwa, sasa umefupika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Hivyo zile danadana, kukosa kuwajibika,
Huko Kagera hapana, watu watawajibika,
Kazi kwao kukazana, maji kwa watu kufika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Ni faida kubwa sana, mradi kukamilika,
Vile kaya nyingi sana, ambako yatatumika,
Wananchi wengine sana, kweli wamefarijika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Serikali mepania, huduma maji kufika,
Kotekote Tanzania, miradi inafanyika,
Wanawake Tanzania, wapate kupumzika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Maji yanavyosambazwa, kwa wananchi kufika,
Na wao wameelezwa, lazima kuwajibika,
Bili bila bambikizwa, kulipa wanahusika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Awamu hii ya Sita, kweli inachakarika,
Magumu kufutafuta, ahueni kutufika,
Maji ona tunapata, miradi kikamilika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Pamoja kulipa bili, vile limeelezeka,
Pia ulinzi kamili, wa miradi twahusika,
Kusitokee tumbili, hiyo ikahujumika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

>Miradi tukiilinda, vizuri ikatumika,
Taifa tunalipenda, ukarabati washuka,
Mbele tutazidi kwenda, pesa vema kitumika,
Ni ndani ya siku saba, maji yafike kwa watu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news