OR-TAMISEMI yatoa maagizo kwa halmashauri zilizokamilisha majengo ya upasuaji

NA OR-TAMISEMI

TIMU ya Usimamizi Shirikishi kutoka Idara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Seali za Mitaa ( OR-TAMISEMI) imezitaka halmashauri zote nchini ambazo zimekamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanza kutoa huduma hiyo mara moja ili kuwaondolea wananchi hadha na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo maeneo mengine jirani.
Wito huo umetolewa leo Juni 1, 2022 na timu hiyo ilipofanya ziara ya usimamizi shirikishi wa kukagua utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya , pamoja na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za afya katika Mkoa wa Lindi.

Akizungumza kwa niaba ya timu hiyo, Bw. Mathew Maganga ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Dawa Ofisi ya Rais-TAMISEMI amesema kuwa, kumekuwa na ucheleweshajiwa kuanza utolewaji wa huduma za afya hasa huduma ya upasuaji wakati miundombinu ya kutolea huduma hiyo inapatikana, hivyo ametoa wito kwa halmashauri zote nchini kuchukua hatua stahiki na kuanza utekelezaji huo sio zaidi ya Juni 30, 2022.
“Utakuta ujenzi wa jengo la upasuaji umekamilika,watumishi wapo na vifaa tiba vipo, lakini bado huduma haijaanza kutolewa, huduma hii inatakiwa mara moja ili tuwasaidie wananchi hasa wanawake kuondokana na hadha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma,” amesema Bw. Mganga.

Aidha, Bw.Mganga ametoa wito kwa Timu za Usimamizi wa Shughuli za Afya (CHMT) katika Mkoa wa Lindi kuendelea kuihusisha jamii katika utekelezaji wa miundombinu ya kutolea huduma za fya ili kuleta uelewa wa pamoja na kuongeza nguvu kazi na umiliki wa wananchi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Serikali pekee haiwezi,tunahitaji nguvu za wananchi katika kusimamia miradi hii ili kukamilisha kwa wakati na kwa ubora zaidi, lakini pia nguvu kazi ya jamii inasaidia kupunguza gharama za utekelezaji na akiba ipatikanayo kupitia nguvu za wananchi kusaidia kutumika katika nyongeza ya miradi mingine kama vile vichomea taka na placenta pit,"amesema Bw. Maganga.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Kheri Kagya ameahidi kabla ya kufika Juni 30,mwaka huu utekelezaji huo utaanza mara moja kwa vituo vyote ambavyo vimemaliza ujenzi wa jengo la upasuaji katika Mkoa wa Lindi ili kuwaondolea wananchi hadha hiyo.

Katika Mkoa wa Lindi timu ya usimamizi shirikishi imetembelea na kukagua utekelezaji wa miundombinu katika Hospitali ya Wilaya ya Mtama,Kituo cha Afya Nandagala,Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

2 Comments

  1. Hongereni timu ya Mtama Lindi kwa usimamizi mzuri wa miundombinu ya hospitali ya wilaya na vituo vya kutolea huduma.

    ReplyDelete
  2. Kusifiana na kiutendaji sasa. Wapewe haki zao pia hao watumishi ili wajitume zaidi
    . Halmashauri nyingi wanachelewesha sana haki za msingi hasa hasa malipo ya haki zao. Wahasibu wa idara wanahitaji msaada mkubwa na wengine wabadilishwe wameshiba sana.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news