Royal Tour kuwakutanisha Watanzania 1,000 jijini Mwanza

NA DIRAMAKINI

SERIKALI mkoani Mwanza imeanika faida zinazotokana na Filamu ya The Royal Tour kuwa itachochea ongezeko la watalii,pato la taifa, kukuza utalii na uwekezaji katika sekta mbalimbali.  
 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema, filamu hiyo itaoneshwa mkoani humo Juni 18, mwaka huu katika ukumbi wa Rocky City Malls na kutazamwa na wananchi zaidi ya 1000.
Amesema, tukio hilo ni muhimu katika kuunga mkono juhudi na kazi kubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kutangaza utalii pamoja na utamaduni wa Tanzania,pia kuutangaza Mkoa wa Mwanza kama lango kuu la utalii kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye vituvio vingi vya utalii.

Mhandisi Gabriel amesema kuwa, filamu hiyo hadi sasa imetazamwa na watu lukuki wa mataifa mbalimbali duniani,itaongeza watalii wanaotembelea nchi yetu,pato la nchi litaongezeka sambamba na uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Pia kuongezeka kwa watalii kutawezesha wafanyabiashara wa sekta hiyo kuingiza vipato maradufu wakiwemo wamiliki wa kampuni za utalii na wasafirishaji,huduma za malazi na chakula vikiwemo vya asili, wauza sanaa na bidhaa mbalimbali za utamaduni,wauzaji wa vito vya thamani na waongoza watalii watapata vipato kupitia biashara hizo.

Alisema, filamu hiyo ya The Rayol Tour itakuza utalii wa ndani na tangu ianze kuonyeshwa wananchi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mwanza na maeneo mengine nchini,itahamasisha vijana na wanawake kubuni na kuanzisha biashara katika sekta ya utalii na kujipatia kipato na familia zao.

“Kanda ya Ziwa kuna vivutio vya utalii kama hifadhi za taifa,mapori tengefu,Ziwa Victoria,miamba ya mawe likiwemo Jiwe la Bismark Rocky,maeneo ya kihistoria,utalii wa utamaduni wa asili,michezo,maji,utalii wa misitu na makumbusho ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Butamaa,”alisema Mhandisi Gabriel.

Aliongeza kuwa, filamu hiyo ya kwanza kutengenezwa na Rais na Kiongozi Mkuu wa Taifa letu itakuza uelewa wa wananchi na kuwahamasiha kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi za taifa na vivutio vya ndani na nje ya Mwanza,itatambulisha Mkoa wa Mwanza kuwa lango kuu la kuingilia Hifadhi ya Serengeti na itawachukua watalii saa 2:30 kufika katika hifadhi hiyo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, kabla ya filamu hiyo kuonyeshwa Juni 18,mwaka huu majira ya saa 9:00 hasi saa 1:00 jioni,Juni 16 wananchi 150 kutoka mkoani humu watatembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Pia Juni 17,kutakuwa na ziara ya kufanya safari za ziwani (boat tours) kutembelea vivutio vya utalii Jiji la Mwanza vya Hifadhi ya Saanane,Jiwe la Bismark,Gunzet House na Makumbusho ya Kabila la Wasukuma Bujora.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hafadhi ya Kisiwa cha Saanane, Eva Mallya alisema wanamshukuru Rais Samia kwa jitihada za kuandaa filamu hiyo ili kuitangaza Tanzania kimataifa,pia Mkuu wa Mkoa,Mhandisi Gabriel kuitambulisha kwa wananchi.

Alisema, The Royal Tour italeta mwamko kwa watalii wengi wa ndani na nje kuja kutembelea hifadhi zetu za Saanane,Serengeti,Ibanda-Kyerwa,Chato-Burigi na Rubondo ambapo wamejindaa kuwapokea na wataendelea kuboresha vivutio vya utalii vilivyo ili kuvutia zaidi wageni.

Naye mdau wa utalii wa ndani, Mhandisi Mnandi Mnandi alishauri serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii,kupunguza ada ya kuingia hifadhini kwa watalii wa ndani na wananchi wa kipato cha chini kumudu gharama hizo.

“Wananchi wengi hasa wa kipato cha chini wanatamani kutembelea hifadhi lakini wanashindwa sababu ya gharama,ni rai yangu serikali ione namna ya kupunguza tozo hizo ili wananchi hao pia wanufaraike kwa kuziona rasilimali zao za wanyama na vivutio vingine,”alisema Mhandisi Mnandi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news