SENSA NI WAJIBU WETU:Kwa mazuri matokeo, idadi ichukuliwe

NA LWANGA MWAMBANDE (KiMPAB)

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya Sensa hiyo.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,ifikapo Agosti 23 hakikisha unahesabiwa na unahesabiwa mara moja tu kwenye kaya uliyolala usiku wa kuamkia siku ya sensa, zaidi jifunze kupitia shairi hapa chini;

A:Sensa ni wajibu wetu, twende tukahesabiwe,
Sensa makazi na watu, ni vema itambuliwe,
Agosti shinatatu, sisi sote tufikiwe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

B:Rais kule Missenyi, asema tuhesabiwe,
Ni wito wetu na ninyi, idadi ichukuliwe,
Tunduru, Kyerwa, Malinyi, budi sote tufikiwe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

C:Sensa kwetu ni muhimu, zile takwimu tupewe,
Makundi tuyafahamu, idadi yao tupewe,
Wanawake wetu humu, hata waume wenyewe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

D:Mahitaji maalumu, ili huduma wapewe,
Ni rahisi si vigumu, zile takwimu tupewe,
Sote tutashika zamu, ya kwao yatatuliwe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

E:Kupanga maendeleo, si huruma uonewe,
Kwa mazuri matokeo, idadi ichukuliwe,
Kusiwe upendeleo, na huduma zitolewe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

F:Zoezi sensa ni letu, sisi sote tufikiwe,
Maswali ya sensa yetu, sisi sote tupitiwe,
Tena kwa utashi wetu, na majibu yatolewe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

G:Mepita miaka kumi, tangia tuhesabiwe,
Zile takwimu uvumi, mwaka kesho situmiwe,
Tufanye mambo kisomi, hizi mpya zitumiwe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

H:Wananchi wote shime, twende tukahesabiwe,
Maelekezo tusome, kifike tusichelewe,
Kila mtu ajitume, asojua aambiwe,
Sisi sote twahimizwa, muhimu kuhesabiwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments