SERIKALI KUONGEZA WIGO ZAIDI WATANZANIA KUSOMA NCHINI MAREKANI-WAZIRI MKENDA

NA MATHIAS CANAL, WEST

SERIKALI imesema kuwa itatangaza fursa zaidi kwa ajili ya watanzania wengi kusoma nchini Marekani na nchi nyingine kote Duniani.
Miongoni mwa maeneo ambayo serikali inakusudia kuyawekea mkazo kwa wananchi kusoma nje ya nchi ni pamoja na eneo la Sayansi, Teknolojia na elimu tiba.

Utekelezaji wa matakwa hayo ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 pamoja na mkakati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha yanafanyika maboresho ya elimu nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 7 Juni 2022 ofisini kwake jijini Dodoma wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donard Wright.

Waziri Mkenda amesema kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo kwa watanzania kusoma nje ya nchi ni kuimarisha mageuzi ya elimu ambayo serikali ya awamu ya sita imekusudia kuyafanya hususani katika elimu ya ufundi na elimu ujuzi.
“Ni maelekezo ya Rais wetu kuhakikisha elimu inayotolewa inamuandaa mtoto kwa ujuzi, kwa hiyo kwa sasa tunapitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala ili iweze kukidhi mahitaji hayo,”amesema Prof. Mkenda.
Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt.Donard Wright amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa nchi yake ipo tayari na itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya elimu ili kuhakikisha ubora wa elimu kwa kila mtoto kwani elimu ndio mkombozi kufikia malengo endelevu.

Post a Comment

0 Comments