TIRA yapata suluhu ulipaji mafao ya bima wanufaika 203 NCAA, yatoa adhabu kali

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) imesema imefanikiwa kupata suluhu ya ulipaji wa mafao ya bima kwa zaidi ya wanuifaka 203 ambao ni wakata bima (Policyholders) watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA). 
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Bima,Dkt.Baghayo A.Saqware wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusu maamuzi ya ulipaji wa mafao kwa wanufaika wa Mfuko wa Bima ya Maisha (Group Endowment Assurance Scheme) kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Kamisha Dkt.Saqware amesema wafanyakazi hao walionyimwa na kukosa haki yao kwa zaidi ya miaka nane toka mwaka 2014. 

Aidha, amesema maamuzi hayo yanalenga kulinda haki za wateja wa bima na kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Saqware amesema amesema, mwaka 1994, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ilianzisha mfuko wa bima ya maisha ili kutoa mafao kwa wafanyakazi wake wanapostaafu ama kufariki. 

Mfuko huo amesema, unasimamiwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kupitia kwa kampuni ya Ushauri wa Bima iitwayo Intertrade Express Limited.

Amesema, Septemba 21,2020 alipokea malalamiko kutoka kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwamba Shirika la Bima la Taifa (NIC) wameshindwa kulipa mafao kwa wanufaika wa mfuko kwa wakati na Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade Express Limited imeshindwa kutoa ushauri sahihi wa kibima na kwa uweledi kwa mujibu wa Sheria ya Bima na Miongozo yake.

"Kati ya Septemba 2020 hadi Oktoba 2021, Baada ya kupokea malalamiko hayo, Mamlaka ilifanya mawasiliano, mahojiano na ukaguzi maalumu ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo.

"Mnamo tarehe 20, Oktoba 2021, Kamishna aliunda kamati maalum na kuipa hadidu za rejea 15 ili kuhakikisha malalamiko hayo yanapatiwa ufumbuzi. Kamati ilifanya kazi kuanzia siku ya Jumatatu ya tarehe 25 Oktoba, 2021 na kuwasilisha taarifa kwa Kamishna siku ya Jumatatu ya tarehe 1, Novemba, 2021. 

"Wajumbe wa kamati hiyo walitoka TIRA, NCAA, NIC na Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade Express Limited.Baada ya kupokea na kuchambua taarifa iliyowasilishwa na kamati,Mamlaka ya Usimamizi wa Bima ilibaini makosa ya ukiukwaji wa Sheria ya Bima SURA Na. 394 na Miongozo inayosimamia biashara ya bima,"amesema Dkt.Saqware.

Aidha, amesema kuwa, makosa yaliyobainika kufanywa na kila mhusika ni kama ifuatavyo;

a. Shirika la Bima la Taifa (NIC)

i. Kutolipa wanufaika wa Bima ya Maisha baada ya Kuiva kwa Bima hiyo kwa mujibu wa mkataba, hivyo kukiuka Masharti na Vigezo vya Mkataba, Kinyume na Sheria ya Bima SURA Na. 394.

ii. Kushindwa kuweka kumbukumbu sahihi za mteja kinyume na kifungu cha 34 (2 (a) (b) cha Sheria ya Bima SURA Na. 394.

iii. Kutoa taarifa za kuridhia (clearance letter) kwa kampuni ya Ushauri ya Intertrade kuwa haina deni lolote ili ipewe leseni na Mamlaka wakati NIC ikifahamu inaidai kampuni hii Tozo za Bima, kinyume na Waraka Na. 97/2021 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima.

b. Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade

i. Kutoa huduma za bima kinyume na Mawanda na matakwa ya leseni waliyopewa na Kamishna kinyume na kifungu cha 161(1) na (2) cha Sheria ya Bima SURA Na. 394.

ii. Kupokea Tozo za Bima kinyume na kifungu cha 72 (2) na (4) cha ya Marekebisho ya Sheria ya Mwaka 2017.

iii. Kutotoa ushauri sahihi kwa kuzingatia uweledi wa kibima kwa mteja kuhusu viwango vya bima kwa mujibu wa skimu husika kinyume na kifungu cha 165 (1)(a),(b)& (c) cha Sheria ya Bima Sura 394.

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro

Kamishna wa Bima,Dkt.Saqware amesema amejiridhisha kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro imeshindwa kuwasilisha michango ya wanachama baada ya kuwakata katika mishahara yao kwa zaidi
ya siku 30 kinyume na Kifungu cha 159 cha Sheria ya Bima Sura 394,kinachosema;

“Any employer who deducts any premiums from any policyholder's salary or emoluments and fails or delays to remit that premiums for a period exceeding thirty days, commits an offence and shall upon conviction be liable to a fine not exceeding two times the amount of the premiums remittance of which is so delayed or to imprisonment for a term of six months or to both,”amesema.

Pia amesema, Sheria ya Bima SURA Na. 394, inampa Kamishna wa Bima Mamlaka ya kutoa adhabu kwa mtu yeyote, kampuni au taasisi itakayobainika kujihusisha na Biashara ya Bima Nchini na kuvunja Sheria ya Bima. 

"Hivyo natoa adhabu kwa Shirika la Bima la Taifa, Kampuni ya Ushauri ya Intertrade Express Limited na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama ifuatavyo:

Shirika la Taifa la Bima.

a. Kulipa wanufaika wote wa skimu ya Bima ya wafanyakazi wa NCAA kwa mujibu wa mkataba na makubaliano ya pande zote yaliyofanyika tarehe 9, Juni 2022. Malipo hayo yaanze kabla au ifikapo tarehe 1 Julai 2022.

b. Kuboresha uendeshaji wa skimu kwa kuweka mfumo madhubuti wa utunzaji kumbukumbu za wateja kwa mujibu wa Sheria ya Bima SURA Na. 394

c. Kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi waliosababisha kutokea kwa makosa kwa uzembe au kwa makusudi na kusababisha usumbufu kwa wateja.

d. Kulipa faini ya Shillingi za Tanzania Milioni Kumi na Tano (15,000,000.00) kwa makosa yote yaliyobainishwa.

e. Kutoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Kamishna kila baada ya miezi mitatu kuanzia tarehe ya tangazo hili.

Kampuni ya Ushauri wa Bima ya Intertrade Express Limited

a. Ninaipiga faini kampuni ya Udalali wa Bima ya Intertrade Express Limited jumla ya Shillingi ya Kitanzania Milioni Mia Moja Sitini na Tano (165,000,000.00) kwa mujibu wa kifungu cha 72(5), 161(1)(2),166(1) cha Sheria ya Bima SURA Na. 394. Kwa makosa yote matatu.

Kuchukuliwa hatua zingine za Kisheria endapo watashindwa kutekeleza wajibu na Masharti kwa mujibu Sheria ya Bima SURA Na. 394.

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro

a. Kuwasilisha Tozo za bima kwa Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.

b. Kamishna wa Bima anatoa adhabu kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ya kulipa faini ya kiasi cha Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Mbili Sitini na Nne Laki Nne Thethini na Tisa Elfu Mia Moja na Tisini na Nane ( 264,439,198) kwa kosa la kushindwa kuwasilisha michango iliyokatwa katika mishahara ya waajiriwa chini ya kifungu cha 159 cha Sheria ya Bima SURA Na. 394 Pamoja na adhabu hizo, natoa rai kama ifuatavyo;

a. Kwa dhati kabisa ninawapongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kuanzisha skimu ya bima za maisha kwa wafanyakazi wake. 

Aidha, ninahimiza taasisi za umma na binafsi kuanzisha mifuko kama hiyo kwa faida ya wafanyakazi.
b. Katika uchunguzi huu kuna viashiria vya makosa ya jinai, hivyo Mamlaka inawasiliana na vyombo vya uchunguzi wa makosa ya jinai kwa hatua stahiki.

c. Ieleweke kuwa hatua hizi zinachukuliwa ili kulinda haki za watumiaji wa bima, kuendeleza soko la bima, kujenga taswira chanya ya soko na kuvutia wawekezaji.

Aidha, Kamishna anawasihi na kutoa onyo kwa Bodi na Watendaji wakuu wa kampuni za Bima nchini kusimamia kwa uweledi na kutokuchelewesha kulipa fidia halali kwa wateja na wanufaika wa bima nchini.

e. Pia, ninawaasa watanzania kuendelea kutumia huduma za bima nchini na kutosita kuleta Malalamiko yao kwa Kamishna wa Bima pindi wanapoona kampuni za bima haziwatendei haki,"amefafanua kwa kina Dkt.Saqware.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news