TRA Geita yakemea upotoshaji Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) Ofisi za Mkoa wa Geita imewataka wafanyabiashara kuondoa dhana potofu juu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) badala yake wanapokidhi vigezo wasajiliwe ili kupata fursa za kiuchumi.
Kauli hiyo inakuja baada taarifa kuonyesha baadhi ya wafanyabiashara waliotimiza vigezo wamekuwa hawana uelewa juu ya VAT na kukwepa kusajiliwa pasipo kujua kodi hiyo inalipwa na mteja na inatoa fursa ya kupata tenda kwa makampuni.

Akizungumza katika maonesho ya Fahari ya Geita katika viwanja vya CCM Kalangalalala mkoani Geita, Ofisa Huduma Elimu kwa Mlipa Kodi TRA Ofisi za Geita, Justine Katiti amesema, VAT haiongezi gharama ya kodi bali inalipwa kwa thamani ya faida ya utoaji huduma kwa mteja.

“Niwaondoe hofu wafanyabiashara kwamba ukisajiliwa kwenye VAT kwamba kunaongeza gharama, (ya kodi) hamna gharama yeyote, sana sana inampa nafasi mfanyabiashara atakapokwenda kununua bidhaa mfano pikipiki atakapokwenda kununua pikipiki atalipa VAT kule.

“Atakapokuja kuuza ile pikipiki atajirejeshea kwanza ile VAT aliyolipa kule alipokwenda kununua ule mzigo kwa hiyo ni faida, unapokuwa umesajiliwa kwenye VAT unapouza ile bidhaa unajirejeshea kwanza ile gharama ya VAT,"amesema Katiti.

Amesema, wafanyabiashara hawapaswi kuamini kwamba wanapolipa tozo za Serikali na VAT wanalipa kodi zaidi ya mara moja kwa kuwa VAT inalipwa na mteja anaponunua bidhaa.

Katiti amewataka wafanyabiashara kuendelea kufanya biashara kwa miongozo ili kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha huduma za kijamii kwa kuwa kodi inayotozwa inarejea moja kwa moja kwenye huduma za kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news