VEMA IBAKI AMANI: Kemea bila kusita, ni ndugu kusiwe vita, EAC Hakuna Matata

NA LWAGA MWAMBANDE

JUMUIYA ya Afrika Mashariki ina nchi wanachama saba, ambazo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Lengo kubwa la jumuiya hii ni kuchagiza maendeleo ya kiuchumi katika nchi hizo zenye zaidi ya watu milioni 300 na kuleta ustawi wa wananchi wake.

Licha ya kuanzisha soko la pamoja, na umoja wa forodha, malengo mengine ya Jumuiya hiyo ni kuwa na sarafu moja na baadaye serikali ya shirikisho. Ni matumaini yetu kwamba malengo hayo yatafikiwa.

Hata hivyo, katika siku za karibuni kumekuwa na chokochoko kati ya nchi wanachama kwa maana ya Rwanda na DRC ambazo hazioneshi taswira nzuri ya jumuiya. Malenga wa kizazi kipya, Lwaga Mwambande, kupitia ushairi anaziasa nchi hizo jirani kuepuka mapigano na badala yake kukumbatia amani.Karibu;


a;Kwenye jumuiya vita, hivyo hatutaki hata,
Kwetu Hakuna Matata, tunaimba tunapita,
Vipi tupigane vita, wenyewe kujiburuta?
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

b:Taarifa zinapita, nchi zinavutavuta,
Lawama zinajikita, huku kwetu twazipata,
Hiyo siyo nzuri hata, siyo vema tukapata,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

c:Silaha kupitapita, na watu kufurukuta,
Kemea bila kusita, ni ndugu kusiwe vita,
Endapo kuna utata, tujitahidi kufuta,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

d:Chonde chonde vita futa, kuaminiana pata,
Tufurahi tukipita, bila ya kusitasita,
Jumuiya tumepata, sote tuweze kupeta,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

e:Kama vikizuka vita, mtaongeza utata,
Kwanu Ukraine vita, shida nyingi tunapata,
Ni bora tukajikita, kupatana tukapata,
Afrika Masharii, vema ibaki amani.

f:Undugu tushaupata, Jumuiya tumepata,
Mashaka tukiyapata, mbele kufika utata,
Amani tukiipata, mambo bora tutapata,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

g:Kutajataja nasita, mnaotishia vita,
Ujumbe mnaupata, hekima bora kuchota,
Futa mipango ya vita, amani bora tafuta,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

h:Nchi moja nazo sita, suluhu bora tafuta,
Kwani kiibuka vita, sote tabu tutapata,
Amani mkiipata, sisi sote tutapeta,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

i:Vita siyo nzuri hata, elimu tumeshachota,
Hata nyumba za ukuta, zinafutwa kama bata,
Watu kama makuruta, wakimbizwa navyo vita,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

j:Mungu na Bwana wa vita, ona huku tunapita,
Si vyetu ni vyako vita, sisi hatutaki vita,
Tuepushe navyo vita, kwetu kusiwe utata,
Afrika Mashariki, vema ibaki amani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news