Viongozi walioteuliwa leo na Rais Samia kuapishwa kesho

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaapisha viongozi wateule aliowateua leo Juni 29, 2022 kesho Juni 30, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bi.Zuhura Yunus leo Juni 29,2022 ambapo uapisho huo utafanyika saa saba mchana.

Uapisho huo utafanyika, baada ya Mheshimiwa Rais Samia kumpandisha cheo Meja Jenerali Jacob John Mkunda kuwa Jenerali na kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (Chief of Defence Forces-CDF).

Kabla ya uteuzi huo,Meja Jenerali Mkunda alikuwa Mkuu wa Tawi la Operesheni na Mafunzo katika Makao Makuu ya Jeshi (Chief of Operations and Training).

Wakati huo huo, Rais Samia pia amempandisha Cheo Meja Jenerali Salum Haji Othman kuwa Luteni Jenerali na amemteua kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (Chief of Staff-Cof S).

Kabla ya uteuzi huo Meja Jenerali Othman alikuwa Kamishna wa Utafiti na Maendeleo Jeshini (Commissioner for Research and Military Development) katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Vile vile amemteua Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule kuwa Balozi ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Post a Comment

0 Comments