Wakulima wa maharage kunufaika na fursa kutoka WFP mkoani Kigoma

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha Ushirika cha Muungano Kiziguzigu Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma kinatarajia kuuza tani 400 za zao la maharage kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na wanunuzi wengine katika msimu huu wa 2021/2022.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Ushirika huo, Jackson Bujege wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea chama hicho na kuona shughuli ambazo wanafanya.

Bujege alisema wakulima wa maharage wameongeza uzalishaji baada ya kupata Mradi wa Kigoma Pamoja Program (KJP), ambapo kwa upande wa kilimo unatekelezwa na WFP, Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC), Shirika la Uendelezaji wa Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Alisema mashirika hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao na masoko hivyo watahakikisha manufaa hayo yanaendelea.

“WFP wamekuja kutukomboa ambapo baada ya mradi kuanza mwaka 2018 walinunua tani 100 za maharage, msimu wa pili tani 368 na msimu huu tunatarajia kuuza tani 400 kwa sh.1950 hadi 2,000,” alisema.

Bujege alisema katika misimu hiyo miwili wakulima ambao ni wanachama wa AMCOS waliweza kuingiza sh.milioni 717, fedha ambazo zimetumika kuchochea shughuli za maendeleo na kilimo.

“AMCOS hii ina wanachama 308 ambapo wanaume ni 200 na wanawake 108, ila tunaendelea kuhamasisha wanachama wanawake kujiunga ili kuweza kuwainua,” alisema.

Alisema mikakati ya chama chao ni kuhakikisha uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 1,000 za maharage.

Ofisa Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Kakonko, Khalfan Muhidin alisema halmashauri hiyo inafurahi ujio wa WFP na mashirika mengine ambapo zaidi ya wakulima 1,800 wamepata elimu kuhusu uhifadhi mazao, mbinu za kulima, kupunguza upotevu wa mazao yakiwa shambani na masoko.

“Wananchi wengi wamehamasishwa kukusanya mazao katika eneo moja, kwani bei yake ni kubwa na wakulima wananufaika,” alisema.

Ofisa huyo alisema ujio wa mradi huo umeongeza mapato kwa halmashauri ambapo mwaka jana wamekusanya ushuru zaidi ya Sh.milioni 21.8 kutoka Sh.milioni tano zilizokuwa zikakusanywa awali.

Alisema wataendelea kutoa elimu kwa wakulima zaidi ya 200,000 walioko kwenye wilaya hiyo, ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji na kujiunga na vyama vya ushirika.

“Lengo ni kuongeza uzalishaji kupitia AMCOS zilizopo ambapo kwa sasa tuna Gwarama, Muungano, Kabingo, Kuchikeka na Kanyonza,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa alisema ujio wa mashirika hayo wilayani kwake umechangia shughuli za uchumi na maendeleo kukua kwa kasi.

Naye Mkuu wa Ofisi ya WFP Kibondo, Saidi Johari alisema katika msimu huu wanatarajia kununua tani 3,000 za maharage kutoka kwa wakulima mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news