Wakutana kupanga mikakati ya kusukuma mashauri Mwanza

NA STEPHEN KAPINGA-Mahakama

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mwanza tarehe 10 Juni, 2022 imefanya kikao cha kusukuma mashauri kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupanga mikakati ya pamoja yenye lengo la kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi. 
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Monica Ndyekobora (katikati) akiongoza kikao cha kusukuma mashauri kilichohudhiriwa na wadau mbalimbali.

Wajumbe wa kikao hicho kilichofanyika katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Buswelu-Mwanza chini ya Mwenyekiti, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Monica Ndyekobora, walianza kwa kujadili mashauri ya jinai yanayoendelea katika Mahakama zote za Mkoa wa Mwanza ambapo ilibainika uwepo mdogo wa mlundikano. 

Katika taarifa yake kwa wajumbe hao, Mhe. Ndyekobora alibainisha kuwa mashauri ya jinai ambayo ni ya mlundikano ni yale ambayo Mahakama haina mamlaka ya kuyasikiliza. 

Hivyo amewapongeza Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya kwa kuondoa mashauri ya mlundikano katika vituo vyao. Alisema, “Kipekee nawapongeza sana Wafawidhi wa Wilaya kwa kushirikia na ofisi ya mashtaka katika Mkoa pamoja na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mwanza kwa kuwezesha hili. Hii inaonesha ni jinsi gani tunavyozingatia agizo la Jaji Mkuu la kuhakikisha mashauri yote ya jinai yanaisha ndani ya muda na hivyo kudhihirisha haki inatendeka kwa wote na kwa wakati.” 

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni Mwendesha Mashtaka Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Afisa Uhamiaji wa Mkoa, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza, Mawakili wa Serikali, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote za Mkoa pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza. 

Katika kikao hicho, wajumbe walifikia mikakati kadhaa ikiwemo kuhakikisha mashauri yote ya jinai yanasomwa maelezo ya wali (PH) ndani ya siku saba tangu shauri kufunguliwa, kusikiliza ushahidi kati ya siku saba na 14, huku utetezi ukitolewa kati ya siku ya 15 na 21 tangu kufunguliwa kwa shauri husika. 

Wajumbe hao pia waliweka msisitizo wa kutoa uamuzi ndani ya siku 60 tangu kufunguliwa kwa shauri husika kwa washitakiwa ambao wapo mahabusu, hatua ambayo itasaidia kuondoa msongamano gerezani. 

Akizungumza katika kikao hicho, Mwendesha Mashtaka Mkuu Mkoa wa Mwanza, Bi Bibiana Kileo aliwakumbusha wapelelezi kuwaruhusu maaskari polisi wanaotakiwa kutoa ushahidi kufika mahakamani kwa muda unaotakiwa na endapo itaonekana kuwa askari husika yupo mbali awezeshwe kutoa ushahidi kwa njia ya “video conference”. 

“Ndugu zangu wa ofisi ya upelelezi kwa hili tunahitaji ushirikiano wa dhati, maana nyie ndio mnahusika na ukamataji, hivyo ni rahisi kujua shahidi kutokana na yale mahojiano mnayofanya. Kwa sasa hatuwezi kukwepa teknolojia, hivyo nawaomba tuondoke kwenye yale mazoea ya zamani ya kuweka vikwazo kwa maaskari pale wanapohitaji ruhusa ya kuja kutoa ushahidi,” alisema. 

Kwa upande wake RCO aliwahakikishia wajumbe wote kuwa ofisi yake itashirikiana vyema na ofisi ya mashtaka pamoja na Mahakama kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati kwa wote. 

“Upande wa ofisi ya upelelezi kwa sasa nasi tunakimbia pamoja na teknolojia ikiwa pamoja na kuwapatia mafunzo maafisa wetu, hivyo ni imani yangu kuwa tukiwa na mawasiliano baina ya ofisi ya upelelezi na ofisi ya mashtaka hakuna shahidi atakayekwama kufika mahakamani, cha msingi wito kwa mashahidi utolewe mapema na tuepuke kuwashtukiza, kwani huenda wakawa wamepangiwa majukumu mengine kama wito haukutolewa mapema,” alisema. 

Naye mwakilishi wa mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika aliahidi kuwakumbusha mawakili wote kupanga ratiba zao vizuri ili kuepuka kuahirisha mashauri mara kwa mara kutokana na ratiba zao kuingiliana na Mahakama za juu. Kwa upande wa mashauri ya madai, wajumbe hao walijiwekea mkakati wa kuyaendesha kwa mfumo wa vikao na pia kutumia fomu ya maelezo ya shahidi pale inapohitajika kama sheria inavyoelekeza ili kuokoa muda na kupunguza kuahirisha mara kwa mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news