Mahakimu mkoani Dodoma waaswa kuzingatia maadili

NA STANSLAUS MAKENDI-Mahakama

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu amewaasa Mahakimu wa Mahakama za Mkoa wa Dodoma kuelewa na kuzingatia Kanuni za Maadili za Maafisa wa Mahakama (Code of Conduct and Ethics for Judicial Officers, 2020 (Government Notice 1001 of 2020) kwa kuwa ni miongoni mwa miongozo muhimu katika kutekeleza majukumu yao. 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu akifafanua jambo wakati wa uwasilishaji wa mada ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama kwa Mahakimu wa Mkoa wa Dodoma walioshiriki mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC Dodoma).

Kiongozi huyo aliyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya ndani yaliyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwaleta pamoja Mahakimu wote wa Mahakama za Mkoa wa Dodoma. Mafunzo hayo yalifanyika mkoani humo jana tarehe 10 Juni, 2022 kwa lengo la kushirikishana, kubadilishana ujuzi, kukumbushana majukumu na viwango bora vya utendaji kazi. 

Sambamba na hilo, Mhe. Mdemu akamtaka Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kusimamia maadili ya Mahakimu katika vituo vyote ndani ya Mkoa huo. 
Picha ya pamoja ya sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo; ikijumuisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma (Mhe. George Masaju, Mhe. Adam Mambi na Mhe. Abdi Kagomba waliokaa), Naibu Wasajili, Mtendaji wa Mahakama na sehemu ya wawakilishi kutoka Mkoa wa Singida.

“Licha ya kuwa tupo viongozi wengine tunaosimamia maadili ndani ya Kanda yote, ninakutaka Mhe. Janeth Musaroche katika nafasi yako ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kusimamia maadili ya Mahakimu katika vituo vyote ndani ya Mkoa,”alisema.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Janeth Musaroche akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mdemu mara baada ya kuhitimisha uwasilishaji wa mada katika mafunzo hayo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhe. Musaroche alitoa wito kwa Mahakimu hao kuzingatia viapo vya kazi zao, kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa sambamba na kuzingatia maelekezo yanayotolewana viongozi na yale yanayotolewa na Mahakama za juu kuhusu mamlaka waliyonayo katika upokeaji na usikilizaji wa mashauri, utekelezaji wa hukumu pamoja na kuimarisha mifumo ya masijala. 

Amesema kuwa, kwa kufanya hivyo kutaongeza kasi katika upokeaji, ufunguaji na usikilizaji wa mashauri na kuyatolea uamuzi kwa wakati ili kuwezesha wananchi kupata haki kwa wakati.
Picha ya pamoja ya sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo, ikijumuisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Naibu Msajili na sehemu ya Mahakimu walioshiriki katika mafunzo hayo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha maadili katika utendaji kazi na hatimaye kuboresha zaidi huduma za Mahakama zinazotolewa katika ngazi zote za Mahakama nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news