Watoto 965,229 wamepewa chanjo ya polio mkoani Mwanza

NA SHEILA KATIKULA

JUMLA ya watoto 965,229 chini ya miaka mitano mkoani Mwanza wamepewa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio iliyotolewa kwa njia ya matone.
Akizungumza na DIRAMAKINI,Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kiteleja amesema, kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio ulianza mei 18 hadi 21, mwaka huu

Amesema, lengo la Serikali lilikuwa kuchanja watoto 846,773 lakini kutokana na wananchi kupata elimu juu ya chanjo hiyo zoezi hilo lilifanyika kwa asilimia 114.
Amesema, kabla ya kampeni hiyo kuanza wahudumu wa afya walitoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa chanjo hiyo.

Amesema, zoezi la utoaji wa chanjo ya polio lilitolewa na wahudumu wa afya na lilifanyika kila sehemu ikiwemo sokoni kwenye vituo vya afya, nyumba kwa nyumba,na kwenye taasisi mbalimbali.

"Serikali inawajali wananchi wake ndiyo maana hatukuishiwa chanjo kwenye zoezi hili na tulifanikiwa kuwafikia watoto wote,"amesema.
Amesema, lengo la chanjo hiyo ni kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini kwa sababu una madhara katika jamii na kupelekea Serikali kuyumba kiuchumi.

"Tumetoa chanjo hiyo ili kuwakinga na kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini kwa sababu una madhara kwani mtoto akipata ugonjwa huu anaweza kupata ulemavu na kufaliki.

"Ugonjwa wa polio unasababishwa na virusi vya ugonjwa wa polio ambavyo humwingia mtu baada ya kushika sehemu ambayo ina kirusi hiki, kula chakula, kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha mtu ambaye ana ugonjwa huu, kwani hauna tiba ila una kinga na ikitokea mtu ana tatizo hili tunatibu dalili zinazojitokeza ndiyo maana tunatoa chanjo ili kuziua usiingie nchini,"amesema.
"Tunashukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ,Wakuu wa wilaya , viongozi dini na viongozi wa mitaa kwa kuelimisha wananchi kwenye zoezi hili na kupelekea watu kujitokeza kwa wingi na kuvuka lengo lililotarajiwa,"amesema Kiteleja.

Kwa upande wake Amina Juma ameishukru Serikali kwa kutoa elimu ya chanjo ya polio na kusababisha wazazi na walezi kuona umuhimu wa kampeni hiyo na kujitokeza kwa wingi kuwaleta watoto wao kupata huduma hiyo.

Post a Comment

0 Comments