Waziri Dkt.Mabula atoa agizo kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kuhusu eneo la mradi wa mgodi wa Nyanzaga

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amemuagiza Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha kukamilisha uthaminishaji fidia kwenye eneo la mradi wa mgodi wa Nyanzaga uliopo Sengerema mkoani Mwanza baada ya wananchi wa eneo hilo kuelewa taratibu za fidia kwenye eneo hilo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa (wa pili kulia) na Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha (Kulia) wakati wa ziara ya kufuatilia program ya kuhamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza Juni 9, 2022. 

Mgodi wa Nyazaga unaoendeshwa kwa njia ya ubia kati ya kampuni ya OreCorp Tanzania Limited (84%) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (16%) upo kata ya Ngoma kwenye vijiji vya Sota na Nyabila na kufunguliwa kwake kunaenda sambamba na zoezi la utwaaji ardhi kwa eneo lote lililoidhinishwa katika leseni ya uchimbaji madini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati wa kufuatilia program ya kuhamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga Juni 9, 2022.

Changamoto katika programu ya kuwahamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga lenye ukubwa wa ekari 5,683 ni baadhi ya wananchi wachache kutoridhika na kiasi cha kiwango kilichoidhinishwa kutumika katika malipo ya fidia ya ardhi na uwepo wananchi wanaodai kuwa na haki ya umiliki maeneo ya milima. 

Hata hivyo, tayari wananchi 1,236 sawa na asilimia 85 wamechukua form namba tatu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kulipwa fidia kupisha program ya kuanza kwa mradi wa mgodi wa Nyanzaga na wananchi 216 sawa na asilimia 15 bado hawajachukua form hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula aliyekwenda kutoa ufafanuzi wa fidia kwa watu wanaotakiwa kuhamishwa katika eneo la mgodi huo, kwa wale wananchi waliokubali kuchukua fomu namba tatu taratibu za kuthaminishwa zikamilishwa haraka ili waweze kulipwa fidia na wale wasiokuwa tayari taratibu za uthamini ziendelee mpaka watakaporidhika.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayupo pichani) wakati wa ziara ya kufuatilia program ya kuhamisha watu na makazi kwenye eneo la mgodi wa Nyanzaga Juni 9, 2022.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati wa kufuatilia zoezi la kuwahamisha watu na makazi kwenye mgodi wa Nyazaga Juni 9, 2022, Dkt.Mabula alisema, uamuzi wa serikali katika kulipa fidia ya kuwahamisha wananchi wa eneo hilo umezingatia taratibu zote za kisheria zikiwemo za kimataifa na hakuna mtu atakayepunjwa au kukopwa.

"Mthamini Mkuu wa Serikali alifanya mapitio na kuongeza kiasi cha malipo ya fidia ya ardhi hadi milioni mbili kwa ekari moja sambamba na aina ya miti nane kufanyiwa kazi kwa miti mitano kuongezwa katika jedwali, miti mitatu imeongezwa kiasi cha kiwango cha malipo,"alisema Dkt.Mabula.
Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha akizungumza wakati wa wa ziara ya ufuatiliaji program ya kuhamisha watu na makazi kwenye eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerma mkoani Mwanza Juni 9, 2022.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Dkt. Steven Kiruswa katika ziara hiyo aliwaeleza wananchi wa kijiji cha Sota kuwa, tamko la sera ya ardhi linaeleza wazi kuwa maeneo ya milima hayapaswi kumilikiwa na mtu binafsi na zaidi ya sera maeneo hayo yanapaswa kulindwa hivyo ni maeneo ya umma.

"Kama kuna mtu yeyote anamiliki mlima na mwenye hati tutakuwa tayari kumlipa, maana sera inaeleza wazi kuwa maeneo ya milima hayapaswi kumilikiwa na mtu ni maeneo nyeti,"alisema Waziri Dkt.Mabula.
Silivester Kahindi, mkazi wa kijiji cha Sota kata ya Igalula wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza akiuliza swali wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula na Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa kufuatilia programu ya kuhamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga Juni 9, 2022.

Aliwatahadharisha wananchi kuhusu maendelezo kwenye eneo la mradi maarufu kama TEGESHA kwa lengo la kutaka kulipwa fidia huku kukiwa na tarehe ya mwisho ya katazo la kufanya maendelezo.

Utegeshaji katika eneo hilo la mradi wa Nyanzaga umefanyika kwenye mazao aina ya alovera, katani, mibono, nanasi na migomba, miti mfano mikalibea na mikaratusi pamoja na utegeshaji wa nyumba mfano ujenzi wa nyumba mpya mahali palipokuwa nyumba ya zamani.

"Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza asingependa kuona migogoro katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa unaonufaisha watanzania" alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa akizungumza katika ziara ya ufuatiliaji program ya kuhamisha watu na makazi kwenye eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerma mkoa wa Mwanza Juni 9, 2022.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Dkt Steven Kiruswa alisema, kuna fursa nyingi zitakazopatikana baada ya mradi mkubwa wa mgodi wa madini ya dhahabu wa Nyanzaga kuanzishwa.

"Fursa zitakazopatikana baada ya mgodi kuanza zitawasaidia wananchi wa kijiji cha Sota na nimpongeze muwekezaji ambaye kabla ya kuanza kazi ameanza kuisaidia jamii ya kijiji hicho hata kabla kuwekeza,"alisema Dkt.Kiruswa.

Alimtaka mwekezaji kuandaa mpango kazi utakaonesha kila mwaka atachangia kiasi gani katika maendeleo ya eneo la mradi huku akibainisha moja ya faida watakayonufaika wananchi wanaoishi eneo la kuzunguka mgodi ni fursa ya ajira.
Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa Nyanzaga wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula na Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa wakati wa ziara ya kufuatilia programu ya kuhamisha watu na makazi kwenye eneo la mgodi wa Nyanzaga Juni 9, 2022.

Moris Omoro mkazi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema ambaye ni mlemavu wa miguu alieleza kuwa, bado hajapata uhakika wa ajira kwa watu wenye ulemavu na kuomba muwekezaji wa mgodi kufikiria namna ya kuwapatia ajira pale mgodi utakapofunguliwa.

Naye mkazi mwingine wa kata ya Igagula Rebecca Wajihi alieleza kuwa, wanachotegemea baada ya kuanzishwa mgodi anaamini wananchi wataondoka kupisha mgodi na kuachia maeneo na sasa wanachotegemea ni vijana kupata ajira ili waishi katika maisha mazuri.
Mkurugenzi Mtendaji na Mshauri Mkuu wa Mazingira katika Kampuni ya DHAMANA Consulting Nanette Bi. Hattingh akielezea namna mradi wa Mgodi wa Nyanzaga utakavyofanyika wakati wa ziara ya kufuatilia program ya kuhamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza Juni 9, 2022.

Eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerema limegusa sehemu ya vijiji viwili vya Sota na Nyabila ambapo jumla ya vitongoji vitano kutoka katika vijiji hivyo vimeguswa ambavyo ni Kaningu B, Kadashi, Sota A, Nyanghona na Nyashimba.
Afisa Usalama wa HSE Consultant Mary Clement akielezea taratibu za kiusalama kwenye mgodi wa Nyanzaga wakati wa ziara ya kufuatilia program ya kuhamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza Juni 9, 2022. Wa pili kushoto ni Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula na kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news