Waziri Mkuu:Shirikianeni kuwalinda watoto wote

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wazazi na walezi washirikiane na walimu katika kuwalinda watoto wa kike na wa kiume ili waweze kutimiza ndoto zao kielimu.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watoto hao wasikubali kudanganywa na watu wasiopenda maendeleo yao na badala yake wasome kwa bidii na wahakikishe malengo yao kielimu yanatimia.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishirIki katika ujenzi wa msingi la Kituo cha Afya cha Namichiga kwenye eneo la Mbuyuni wilayani Ruangwa, Juni 3, 2022. (Pcha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ameyasema hayo Juni 3, 2022 alipozungumza na wanafunzi, wazazi na walimu katika shule ya Sekondari Mandarawe wilayani Ruangwa akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo.

“Kwa sasa kielimu wilaya yetu imepiga hatua kubwa, wanafunzi someni kwa bidii na Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inawawezesha kutimiza malengo mliyojiwekea.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Kata zote za Wilaya hiyo zina shule za sekondari na tayari wameanza ujenzi wa mabweni, lengo likiwa ni kuwapunguzia wanafunzi adha ya umbali mrefu kwenda shuleni.

“Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule apelekwe shule na elimumsingi inatolewa bila ada nchini kote.”

“Kwenye suala la elimu tumejipanga vizuri na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametuunga mkono kwa kutupa sh. milioni 700 za ujenzi wa shule ya sekondari wasichana ya mchepuo wa Sayansi.”

Pia, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Namichiga na ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi wasimamie vizuri mradi huo na wahakikishe fedha zinatumika vizuri.

Mbali na kukagua ujenzi wa kituo hicho, pia Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo vya Afya cha Kata ya Narungombe pamoja na maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Nangurugai.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wananchi wahakikishe wanatunza mazingira na kuacha kukata miti hovyo. “Tutunze mazingira na tusilime katika vyanzo vya maji.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news