'Ati halmashauri kuna mchwa'

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIKU moja niliingia kanisani kusali, nikiwa katika misa hiyo ya asubuhi, wakati inakaribia kumalizika, alisimama kiongozi mmoja kusisitiza waamini kutoa michango kwa ajili ya kurekodi nyimbo za kwaya za kanisa hilo.
 
Michango ilianza kutolewa na watu kadhaa kwa kuinuliwa kutoka katika mabechi ya kanisa hilo. Waamini hao walichangia fedha na kutoa ahadi mbele ya kanisa hilo. Miongoni mwa waliosimamishwa alikuwepo kijana mmoja aliyevalia koti lake nadhifu, alipotakiwa kutaja mchango wake, aliuliza kwa sauti ya kunong’ona na staha kubwa bila ya kutumia mikorofoni.

“Jamani kuna wakati tulichangia fedha za kutosha za kurekodi, je fedha hizo hazikurekodi nyimbo?” Kwa kuwa nilikuwa jirani niliyasikia maneno hayo.

Mwanakwetu kanisani palikuwa kimya, kwa dakika kadhaa, huku viongozi kadhaa wa kwaya wakitoa majibu kwa ndugu huyo kwa kunong’ona. Mwenyekiti wa kanisa hilo naye alitolea ufafanuzi na kama haitoshi hata kiongozi wa kiroho alifanya hivyo pia.

“Jamani waamini wanapotoa michango ni vizuri kuambiwa hata matumizi ya fedha hizo bayana.” Alisisitiza kiongozi huyo wa kiroho akihitimisha ibada.

Tukio hilo la jamii kuwa na hamu ya kufahamu matumizi ya fedha zao kila michango inapofanyika lilimenipa ari ya kuandika matini hii juu ya uwazi katika mambo ya umma, ndiyo maana hoja za kufanyika ukaguzi zinakuwa na umuhimu katika taasisi kadhaa, ziwe za umma au binafsi. Ukaguzi huo unaweza kuwa wa ndani, ukaguzi wa nje na hata ukaguzi maalumu.

Ukaguzi maalumu ni aina ya ukaguzi unaofanyika baada ya kufanyika ukaguzi wa kawaida, hapo sintofahamu fulani inaweza kuibuka labda haikubainika katika ukaguzi wa ndani, kwa hiyo huo ukaguzi maalumu unafanyika kujibu sintofahamu hiyo. Ukaguzi huu unakuwa tafauti na ule ukaguzi kawaida kwa kuwa unakwenda ndani zaidi.

Mathalani vinakaguliwa vifaa vya ujenzi, ukaguzi wa kawaida utakagua ankara, ankara kifani zote pamoja na hati zingine lakini kwenye ukaguzi maalumu vitakaguliwa vitu vilivyopokelewa, alipokea nani? Au hata vimetumikaje? Kama ni mbao, bati au misumari vinapimwa kwa kuhesabu kimoja baada ya kingine. Kwa mfano bati ya kwanza hadi ya mwisho, mbao moja hadi nyingine na hata msumari mmoja mmoja.

Ukaguzi maalumu mara nyingi huwa ni maombi ya mamlaka za juu kama vile Mkurugenzi Mkuu, MkurugenzI Mtendaji , Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Katibu Mkuu, Naibu Waziri na hata Waziri. Ukaguzi maalumu unaweza kufanywa hata katika Halmashauri au taasisi yoyote labda kwenye idara/ pahala fulani ambapo sintofahamu imeibuka kwa kumtuma mkaguzi wa ndani , kuifany kazi hiyo na mwisho kuipeleka ripoti hiyo kwa mkuu wa taasisi.

Katika kila ukaguzi maalumu huwa wanaletwa watu maalumu kuifanya kazi hiyo, siyo wale wanaofanya ukaguzi wa kila mara. Wale wanaofanya ukaguzi wa kila mara wanakuwa pembeni na wale wakaguzi maalumu huwa ni watu wenye taaluma tofauti kama vile afya, uhasibu, uinjinia na sheria kulingana na ukaguzi huo ulivyo.

“Nakumbuka kuna wakati pahala fulani zilikuwa zinajengwa nyumba za Maafisa Tarafa wakaguzi waliokuwa wakiifanya kazi hiyo ni kutoka mkoani.”

Hili nalikumbuka vizuri sana, kumbukumbu hiyo inathibitisha kuwa katika kila wilaya inakaguliwa. Swali la kujiuliza ni je ripoti za ukaguzi huo zinapokaguliwa zinawekwa katika kitabu cha GAG za kila mwaka ?.

Binafsi sijajaliwa kuziona ripoti hizo za kila wilaya na hata kila mikoa .Kama yupo aliyejaliwa kuziona pengine macho macho ni kumchuzi, aliyeona anaweza kunisimulia kwa ripoti ya ukaguzi ya wilaya moja hali ilikuwaje?

Je? Kwa nini utoaji wa ripoti hizo za ukaguzi unakuwa na changamoto? Faida zipo nyingi kama ripoti hizo zitawekwa wazi kwa jamii ambayo ndiyo mmiliki wa fedha za umma, itajua matumizi ya fedha hizo yakoje? Jamii kama haijui matumizi ya fedha hizo yakoje inaweza kukosa imani. Kama inakosa imani je inaweza hata kutokuwaamini wale waliopo katika ofisi hizo. Je hali itakuwa vipi kama hao wakilizungumzia suala la ukaguzi kwa taasisi zilizo chini yao zinazokaguliwa?

“Pale imepelekwa fedha, lakini imetumikaje? Hatujui. Inawezekana fedha hiyo ikawa imetumika kwa matumizi binafsi, hapo inakuwa ni changamoto kubwa, Inatakiwa taarifa zao zionekane katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za kila mwaka.”

Kuna wakati kijana mmoja mkaguzi wa ndani aliingia katika kikao cha Mwenge wa Uhuru, michango ikakusanywa vizuri sana, huku wananchi wakichangia kwa moyo wao wote, kijana huyo alishauri katika kamati ya mwenge ya manunuzi wataalamu wa ukaguzi waingie ili kusaidia kushauri vizuri ili kama kutafanyika ukaguzi wa hizo fedha mambo yawe mepesi.

“aaaaaaaa achana na hayo mambo yako, ofisi ya Mkuu wa Wilaya huwa haikaguliwi…”

Kijana huyu mkaguzi alipojibiwa hilo aliniambia kuwa hili nalo ni tatizo kubwa.“Halmashauri kuna mchwa wengi wanaotafuna pesa za umma.” Jambo hili linasemwa mno.

Je huko kusipotolewa taarifa zake inawezekana kukawa na misumeno (mchwa wakubwa) kwa kuwa taarifa zake hatuzioni. Kama tunataka uwazi basi uwe kote kote, siyo uwazi upande mmoja tu zote ni mali ya umma.

Hata watu wanaopandishwa vyeo kutoka katika nafasi ambazo hazikaguliwi wakiwa na vyeo vya juu wanadhana kuwa wao hawakosei na hawajawahi kukosea kitu ambacho si kweli. Kama wakikaguliwa na taarifa zao kuwa hadharani jamii inaweza kuwafahamu zaidi watu hao kama walikuwa wanakusanya michango ya mwenge kama ilikuwa inakuwa salama au la.

Namalizia kwa kusema kuwa mkaguzi anatakiwa kuwa mtu huru sana, iwe mkaguzi wa nje au hata mkaguzi wa ndani na ndiyo maana baadhi ya watu wanadhani kuwa hata wakaguzi wa ndani pengine si vizuri kukaa katika jengo moja na taasisi wanayofanyia kazi ni vizuri wawe katika jengo binafsi.

Uhuru huo uwe kama wa yule kijana aliyehoji michango ya kwaya kanisani kujirudia kila mara.

Jamii inafahamu vizuri mambo mengi ya umma kwa hiyo uwazi ni jambo la msingi sana ili kujenga kuaminiana.
makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news