Barwany atoa neno mchakato wa Katiba mpya

NA AHMAD MMOW

ALIYEWAHI kuwa mbunge wa Lindi Mjini mwaka 2010 hadi 2015 kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Salum Barwany ametahadharisha kwamba suala la katiba mpya lisifanyike kwa mihemko ya kisiasa na papara. Bali lifanyike kwa umakini na utulivu mkubwa.
Barwany alitoa ushauri na tahadhari mjini Lindi alipozungumza na DIRAMAKINI baada ya kuombwa aeleze mtazamo na maoni yake kuhusu suala la katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema iwapo kuna nia ya dhati ya kupata katiba mpya ambayo itakata kiu ya Tanzania hakuna sababu ya kuendesha mchakato huo kwa papara na mihemko ya kisiasa. Bali kunahitajika umakini, utulivu na muda wa kutosha bila kuogopa gharama. Kwani bila katiba bora hakuna uchumi imara.

Amesema, kuna umuhimu wa kutengenezwa mfumo mzuri na ratiba sahihi ambayo itazingatiwa katika mchakato wa kupata katiba mpya hatua kwa hatua bila kuharakisha ili kuwahi uchaguzi mkuu.

Barwany alikwenda mbali kwakusema ni bora kusogeza mbele uchaguzi kuliko kuingia kwenye uchaguzi huo kukiwa na katiba ya sasa.

"Iwapo muda wa miaka mitatu uliobaki utatosha kupata katiba mpya basi itakuwa bora. Lakini kama muda uliobaki utakuwa hautoshi basi bora kusogeza mbele kuliko kufanya bora liende ili kuwahi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,"amesisitiza Barwany.

Aidha mwanasiasa huyo amesema katiba ndiyo nyenzo sahihi na imara itakayotumika kupata tume huru ya uchaguzi. Kwani katiba itaeleza muundo wa tume hiyo, nani watakuwa wajumbe wake na mfumo gani utatumika kuwapata wajumbe hao.Amebainisha kwamba, tume huru isiyotokana na katiba bora itasababisha mgogoro.

Kuhusu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuridhia kuwepo na mchakato wa kupata katiba mpya amesema, kuridhia kwa chama hicho sio ushindi kwa vyama vya siasa vya upinzani na wanaharakati waliokuwa wanataka lifanyike jambo hilo. Bali ni ushindi wa wananchi ambao wanahitaji katiba mpya.

Amesema iwapo wananchi wataamini kwamba huo ni ushindi kwa vyama vya upinzani na wanaharakati ni dhahiri kwamba CCM kitajiona kwamba katiba itakayopatikana ni mali yake. Kwa hiyo kinaweza kuingilia mchakato huo kwa maslahi yake.

"Chama Cha Mapinduzi wala serikali havina haki wala mamlaka ya kuwaamuru wananchi kuhusu jambo hilo. Hata kama kimeridhia jambo muhimu, lakini haimaanishi katiba itakayopatikana itatokana na ridhaa yake. Kwani hakina mamlaka hiyo,"amesema Barwany.

Pia alikumbusha kwamba hata kipindi cha kuelekea mfumo wa vyama vingi vya siasa kulikuwa na mjadala mkubwa. Mwisho wa siku CCM kilikubali mfumo huo. Hata hivyo kwa shingo upande. Matokeo yake kipaumbale cha msingi ambacho kingesababisha mfumo wa huo kuwa madhubuti na usio sababisha mnyukano na malalamiko ya uwanja usio tambarale na usawa kwa vyama vya upinzani.

Alikitaja kipaumbele hicho kuwa ni katiba. Kwani ilitakiwa mara tu ya kuanza mfumo wa vyama vingi ingefuatia katiba mpya. Hata hivyo hilo halikufanyika. Hali ambayo imesababisha mfumo huo kuwepo kinadharia. Kwa madai kwamba kivitendo ni kama bado nchi ipo katika mfumo wa chama kimoja.

Lakini pia mwanasiasa huyo alitahadharisha kwamba kusiwepo fikra za kuendeleza mchakato wa awali ambao ulifikia hatua ya kupata katiba iliyopendekezwa. Kwani hakutasababisha kupata katiba bora. Kwa madai kwamba hata katiba iliyopendekezwa ina mapungufu mengi. Kwa hiyo mchakato huo uanze upya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news