Maono ya Rais Dkt.Mwinyi kuhusu Uchumi wa Buluu yaibua wasomi, wasema Zanzibar ipo uwelekeo sahihi

NA DIRAMAKINI

AZMA ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi ya kujenga Uchumi wa Buluu umewaibua wasomi na wataalamu mbalimbali hapa nchini wakipongeza na kusema mafanikio ya utekelezaji wake yataupaisha uchumi na maendeleo ya visiwa hivyo kwa haraka.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2020, Rais Mwinyi aliweka bayana azma ya serikali yake kutumia fursa lukuki zinavizunguka visiwa hivyo zikiwemo fukwe, uvuvi, kilimo cha mwani sambamba na mazao ya baharini.

“Zanzibar imebarikiwa kuwa na fukwe nyingi ambazo ni nzuri kwa uwekezaji wa mahoteli na vivutio mbalimbali kwa utalii. Kinachotakiwa hapa uungaji mkono wa wazanzibari wote katika kufanikisha hilo,” Sadiki Mbarouk Mahamudi alisema na kutaka wananchi wahamasishwe Zaidi kuona fursa hizo.

Bw Mahamudi ambaye ni mbobezi katika masuala ya uchumi na uwekezaji alisema fursa zinazoizunguka Zanzibar ni nyingi sana kuliko Zanzibar yenyewe na hivyo kuipongeza serikali kwa kuliona hilo katika awamu hii ya uongozi.

Dkt.Tasco Luambano ambaye ni Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya alisema uamuzi wa Rais Mwinyi kuunda Wizara Maalumu inayoshughulikia masuala ya Uchumi wa Buluu inatoa tafsiri ya halisi ya maono ya kiongozi huyo katika kuiletea Zanzibar mageuzi stahiki ya kiuchumi.

“Hatua ambazo Rais Mwinyi amezichukua tangu aangie madarakani zimelenga kuibadilisha na kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo. Mwenye macho hapaswi kuambiwa aone kwani Zanzibar ya 2020 siyo ya 2022,” alisema.

Dkt.Luambano ambaye huenda Zanzibar mara kwa mara alipongeza juhudi anazochukua Rais Mwinyi kuhakikisha kuwa mazao na raslimali zinazotokana na bahari zinatumika kuijenga Zanzibar na kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Dkt. Zubeda Salim Abdallah alisema uchumi wa buluu ni njia sahihi ya kujenga uchumi imara kwa Zanzibar kwani kupitia mazao ya bahari, uvuvi na raslimali zote zinazovizunguka visiwa hivyo maisha ya wazanzibari wote yatabadilka kwa haraka.

“Uchumi wa buluu ni msingi wa kujenga sekta zingine za uchumi zikiwemo sekta za utalii na huduma, viwanda, miundombino, mawasiliano ,elimu, afya na nyinginezo nyingi,” alisema Dkt Zubeda ni mhadhari wa uchumi na mwenyeji wa Pemba.

Walimtaka Rais Mwinyi kusimamia maamuzi yake kama alivyofanya Rais mstaafu wa Zanzibar, Dkt.Salmin Amour alipoamua ujenzi wa hoteli alipingwa sana na baadhi ya watu bila kujua matokeo ya baadaye na kwa sasa matunda ya uwekezaji huo yanaonekana ambapo serikali inakusanya mapato mengi kupitia tasnia hiyo.

Hivi karibuni, viongozi wastaafu walikemea habari za upotoshaji kuwa Rais ameuza visiwa kama sehemu ya kumkatisha tamaa na juhudi za serikali yake kuhamasisha uwekezaji kwenye fukwe ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo, wastaafu hao walikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa Zanzibar haina madini na kutegemea zaidi uchumi unaotokana mazao ya bahari na kilimo na kumtaka Rais Mwinyi kuendelea kuvutia uwekezaji kwenye fukwe ambao utasaidia kuongeza vipato kwa wakazi wa maeneo husika.

Kauli hizo za viongozi ndani ya chama vimekuja kufuatia baadhi ya viongozi wastaafu ndani ya chama kuleta migongano na mivutano isiyo ya lazima na kushindwa kuwaunga mkono viongozi waliopo waweze kutekeleza majumu yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news