CPB yataja faida za kilimo cha mkataba

NA DIRAMAKINI

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) imesema katika kumuwezesha mkulima kulima kwa tija imetoa mikataba zaidi 6,000 kwa wakulima katika kilimo cha ngano, alizeti na maharage pamoja.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB), Dkt.Anselim Moshi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Kibiashara ya 46 yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam 

Amesema, mkakati huo wa kilimo cha mkataba ulianza mwaka 2020 lengo ni kuhakikisha wakulima wanalima kwa mafanikio.

Dkt.Moshi amesema,mikataba hiyo ilisainiwa na taasisi za kibenki, wakulima, wasambazaji pembejeo, bima pamoja na bodi ya CPB ikiwa ndio mnunuzi mkuu.

"Kwa mfumo huu wa mkataba tunaweza kupata kilimo ambacho ni cha tija kilimo hiki kipo katika Mikoa ya Kaskazini kwa maana ya Kilimanjaro (Siha), Arusha (Monduli, Karatu), Simanjiro na Hanang' Mkoa wa Manyara.

"Katika maeneo haya tumeingia mikataba na wakulima wa ngano, lakini pia tunafanya mkataba kwenye maharage ya Soya na tumeshaanza huko Songea mkoani Ruvuma,"amesema.

Ameongeza kuwa,"mikataba hiyo imekuwa ikitolewa katika zao la alizeti kwenye mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu,"amesema Dkt.Moshi.

Vilevile Dkt.Moshi amesema, CPB inaendelea kujenga viwanda katika mikoa yote nchini ili wakulima wawe na soko la uhakika la mazao wanayoyalima.

Amesema kuwa, viwanda hivyo vitamsaidia mkulima kuwa na soko la uhakika na vinatoa ajira kwa vijana, sambamba na kuongeza thamani kwa mazao yanayolimwa hapa nchini ili kuweza kuuza kwenye masoko ya kimataifa na kupata faida zaidi.

Dkt.Moshi aliendelea kueleza kuwa,dhamira ya CPB ni kuhakikisha mkulima mdogo mdogo nchini anapata bei shindani katika mazao yake.

Aidha, amesema bodi hiyo imejenga uwezo mkubwa wa kuweza kununua mazao ya mkulima na kufanya uchambuzi kujua mkulima anatumia gharama zipi shambani kwa kufanya hivyo mkulima anahamasika kuendelea kulima zaidi na hii inahakikisha kwamba salama wa chakula unakuwepo.

"Serikali imetoa maelekezo kwa bodi hii kuhakikisha kuwa ngano inazalishwa hapa nchini hadi kufikia tani milioni moja na zaidi ifikapo 2025,"amesema.

Amesema, katika kutekeleza mkakati huo mwaka 2021 waliagiza mbegu tani 210 kutoka nchini Zambia na kuzigawa kwa wakulima kwa mkopo katika kanda ya Kaskazini na matokeo yalikuwa mazuri.

Hata hivyo, amesema mwaka huu wamejipanga kwa sababu kuna mbegu zimezalishwa ndani ya nchi na serikali imeweka jitihada kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Kampuni ya Kuzalisha Mbegu ya ASA ili kuweza kuzalisha mbegu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news